Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imejikuta pabaya katika mbio za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, baada ya kufungwa bao 1-0 na Niger katika mechi iliyochezwa Jumanne hii, Septemba 9, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Matokeo ya mechi hiyo ya Kundi E yanaitoa Stars katika ndoto za kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kwani sasa haina nafasi hata ya kucheza play-offs kupitia kundi hilo linaloongozwa na Morocco ambayo tayari imefuzu.
Stars na Niger zote ziliuanza mchezo zikionesha dhamira ya kusaka mabao ya mapema lakini hadi mwamuzi anapuliza filimbi kukamilisha nusu ya kwanza ya mchezo huo hakuna timu iliyopata bao.
Katika kubadili aina ya uchezaji, kocha wa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alianza kufanya mabadiliko mapema kwa kuwatoa Seleman Mwalimu na Yusuph Kagoma na nafasi zao kuingia Mudathir Yahya na Iddi Seleman.
Stars hata hivyo haikuneemeka na mabadiliko hayo badala yake walikuwa Niger waliopata bao kupitia kwa Daniel Sosah aliyeiwahi krosi dhaifu iliyochongwa na Issa Djibrilla.
Katika jitihada za kusaka bao, kocha Morocco aliendelea kufanya mabadiliko safari hii akimtoa nahodha Mbwana Samatta, Feisal Salum na Mohamed Hussein na nafasi zao kuingia Simon Msuva, Abdul Suleiman na Yahya Omar.
Niger ambao walilazimika kucheza 10 uwanjani baada ya mchezaji wao, Katore Abdoulaye kupewa kadi ya pili ya njano na hivyo kuwa nyekundu walionesha umakini wa hali ya juu katika kujihami na kuifanya Stars ishindwe kuutumia upungufu wa wapinzani wao uwanjani kupata bao la kusawazisha.
Stars hata hivyo ilionesha uhai kwa kufanya mashambulizi kadhaa likiwamo moja lililoanzia kwa krosi iliyopigwa na Novatus Dismas na kumkuta Clement Mzize lakini mpira huo haukuweza kuzaa bao.
Baada ya mechi hiyo, Stars sasa inasubiri kucheza mechi yake ya mwisho na Zambia ambayo itachezwa mapema mwezi ujao.
Timu hiyo hadi sasa imejikusanyia pointi 10 ikiwa nafasi ya pili, ikifuatiwa na Niger inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tisa wakati Zambia ina pointi sita na Congo Brazaville ina pointi moja.
Kimataifa Niger yaikwaza Taifa Stars
Niger yaikwaza Taifa Stars
Read also
