El Alto, Bolivia
Baada ya kufungwa bao 1-0 na Bolivia jana Jumanne Septemba 9, 2025, Rais wa Shirikisho la Soka Brazil, Samir Xaud, amelalamikia mazingira ya mchezo huo wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 akidai ni kama walikuwa wakicheza dhidi ya waamuzi, polisi na vijana waokota mipira au ball boys.
Brazil ambao tayari wamefuzu kushiriki fainali hizo, huo ni mchezo wao wa kwanza kupoteza tangu waanze kunolewa na Carlo Ancelotti ambaye alijiunga na timu hiyo mwezi Mei mwaka huu akitokea klabu ya Real Madrid.
Bolivia walipata bao hilo pekee muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Miguel Terceros, bao lililofufua matumaini ya Bolivia kufuzu Kombe la Dunia kwa kuwa sasa imejihakikishia nafasi ya kucheza play off.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Xaud alisema timu yake ilikwenda Bolivia kucheza soka lakini kile ambacho wamekutana nacho mara baada ya kuwasili ni mambo yaliyo kinyume na mchezo huo.
Naye kocha Ancelotti hakufurahishwa na waamuzi wa mchezo huo na wakati timu zikienda mapumziko alionekana kupitia kamera akitoleana maneno na waamuzi katika namna iliyoonekana kama kutokubaliana jambo.
Moja ya mambo ambayo Ancelotti na Xaud wameyalalamikia ni kitendo cha mipira kuingizwa mingi uwanjani wakisema lengo lilikuwa ni kuvuruga mashambulizi ya timu ya Brazil katika mchezo huo hasa dakika za mwisho.
“Tulicheza dhidi ya waamuzi, polisi na ball boys ambao walikuwa wakiitoa na kuirusha mipira uwanjani, ilikuwa balaa tupu, hiki si kitu ambacho unakitarajia katika soka la dunia, tunachotaka ni maendeleo ya soka zaidi ya haya,” alisema Xaud.
Xaud aliongeza kwa kusema kuwa anaamini mamlaka husika za soka zitachukua hatua kwani hata wakati wanawasili Bolivia polisi hawakuwa wema kwao kuanzia timu hadi makocha.
Naye Ancelotti licha ya kutofurahishwa na mazingira ya mchezo huo lakini alisema anataka kuangalia maendeleo ya timu kwa kuyapa umuhimu mambo yajayo na kubwa zaidi ni Kombe la Dunia kwa kuwa lengo lao kuu na anadhani watafanya vizuri.
