Na mwandishi wetu
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia ametoa onyo kwa waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa msimu huu hawatakuwa na mzaha kwa mwamuzi atakayeharibu mchezo.
Karia ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) alitoa kauli hiyo hivi karibuni kwenye ofisi za TFF katika hafla ya kufunga semina ya waamuzi wa ligi kuu.
Kiongozi huyo wa TFF alisema kwamba wanataka msimu huu uwe tofauti akimtaka kilwa mwamuzi kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu.
Akifafanua zaidi Karia alisema kwamba msimu uliopita wa 2024-25 kulikuwa na mtikisiko mkubwa kwa nchi na setikali hivyo katika msimu huu taasisi za serikali zitahusishwa katika kukabiliana na waamuzi wanaoharibu mchezo.
Alisema kwa msimu huu wa 2025-26, kutakuwa na jopo la waamuzi ambao kazi yao ni kujadili matukio ya ligi pamoja na kamati ya waamuzi ambayo itafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya serikali pale inapobidi kwa lengo la kuhakikisha haki inatendeka.
“Huu ni msimu ambao matarajio yetu ni kuwa tofauti, tukimaliza tutapongezana lakini kwa wale wengine ambao watakuwa tofauti hao tutaachana nao moja kwa moja, na katika hili sitanii,” alisema Karia.
Karia hata hivyo aliwapa moyo waamuzi akisema kwamba wana uwezo na ujuzi wa kutafsiri sheria na kwa maana hiyo hawapaswi kuwa chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo ya soka nchini Tanzania.
Alisema kwamba soka la Tanzania limefika mbali kiasi kwamba dunia nzima inatambua hilo na kuwakumbusha waamuzi kuhakikisha hawawi chanzo cha kuliporomosha soka.
