Na mwandishi wetu
Mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amejiuzulu nafasi ya uenyekiti wa bodi ya klabu hiyo na kumteua Crescentius Magori kushika nafasi hiyo.
Taarifa ya Mo iliyopatikana Alhamisi hii Septemba 4, 2025, mwekezaji huyo amesema kwamba kutokana na majukumu mengine yanayomkabili ameamua kuachana na wadhifa wa uenyekiti wa bodi ya klabu hiyo.
Alifafanua katika taarifa hiyo kuwa kutokana na majukumu hayo amejikuta mara nyingi akiwa mbali na shughuli za kila siku za klabu hiyo ingawa alisema ataendelea kubaki na nafasi ya rais na mwekezaji wa Simba.
“Nitaendelea kuwa mwekezaji na rais wa Simba ingawa katika nafasi ya uenyekiti wa bodi nakabidhi kwa kiongozi mpya mwenye muda na ukaribu zaidi,” alieleza Mo katika taarifa hiyo.
Magori si jina geni katika klabu ya Simba kwamba mbali ya kuwa mwanachama wa siku nyingi amewahi kushika nafasi kadhaa ikiwamo ya mtendaji lakini pia alikuwa mjumbe katika kundi maarufu la Friends of Simba.
Sambamba na hilo, Mo pia ametangaza majina ya wajumbe wapya wa bodi ya klabu hiyo wanaotoka upande wa mwekezaji kama katiba ya Simba inavyotaka.
Wajumbe hao ni Barbara Gonzalez ambaye amewahi kuwa ofisa mtendaji katika klabu hiyo, wengine ni Hussein Kitita, Rashid Shangazi, Swedi Mkwabi, George Ruhango, Zuly Chandoo na mfanyabiashara Azim Dewji ambaye pia amewahi kuwa mfadhili wa Simba kwa miaka mingi.
Mo pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wote waliotangulia huku akielezea matumaini yake kwa uongozi mpya katika kuifanya Simba iwe moja ya klabu bora barani Afrika.
