Manchester, England
Kocha wa Man United, Ruben Amorim amesema mpango wake ni kuendelea kuwa kocha wa timu hiyo lakini hana uhakika kama ataendelea na kazi hiyo baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
Kitendo cha timu hiyo kufungwa na timu ya Ligi II ya Grimsby Town katika mechi ya Kombe la Carabao kimezidi kumuweka katika wakati mgumu kocha huyo kutoka Ureno wakati huu mechi za Ligi Kuu England zikiendelea.
Amorim amesema kwamba atafanya kikao na mabosi wa Man United kwa ajili ya kutathmini nafasi yake wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama ana uhakika wa kuendelea na kibarua chake baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, Amorim alisema anadhani mambo hayatabadilika ingawa alisisitiza kwamba hana uhakika wa moja kwa moja katika hilo.
“Sijui nini kitatokea, suala la kubaki hilo ni wazo langu lakini siwezi kuahidi lolote kuhusu mambo yajayo yatakavyokuwa, lakini mimi ni kocha wa Manchester United na hilo haliwezi kubadlika,” alisema Amorim.
Akiizungumzia mechi yao na Grimsby Town, Amorim alisema alichokiona kilimshtua na wachezaji wake bado wanateswa na majeraha ya msimu uliopita baada ya Man United kumaliza katika nafasi ya 15.
Hiyo ni nafasi ya chini kwa timu hiyo kumaliza katika Ligi Kuu England na mara ya mwisho kumaliza nafasi ya chini kama hiyo kwenye ligi kubwa England ni takriban miaka 50 iliyopita.
Amorim alisema anadhani wachezaji wake wakati wote wamekuwa wakifikiria mambo ya msimu uliopita na kusisitiza kwamba wanachotakiwa ni kufikiria mechi ijayo hasa baada ya kupoteza mechi dhidi ya Grimsby.
Kimataifa Amorim yupo njia panda
Amorim yupo njia panda
Read also
