Na mwandishi wetu
Morocco imebeba taji la Ubingwa wa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 baada ya kuilaza Madagascar mabao 3-2 katika mechi ya fainali iliyopigwa leo Jumamosi Agosti, 30, 2025 kwenye Uwanja wa Kasarani, Nairobi, Kenya.
Kwa ushindi huo, Morocco inakuwa timu ya kwanza kulibeba taji la michuano hiyo mara tatu ikiwa tayari imefanya hivyo mwaka 2018 na 2020.
Ushindi huo pia umeiwezesha Morocco kuondoka na kitita cha Dola milioni 3.5 na medali ya dhahabu wakati Madagascar kwa kushika nafasi ya pili wameondoka na Dola 1.2 milioni na medali ya fedha.
Shujaa wa Morocco katika mechi ya leo alikuwa ni Oussama Lamlioui aliyefunga mabao mawili wakati bao jingine likifungwa na Mehri huku mabao ya Madagascar yakifungwa na Manohantsoa na Rakotondraibe.
Madagascar licha ya kupoteza mchezo huo walionesha kila dalili za kutoka na ushindi baada ya kupata bao la kuongoza dakika ya tisa lililofungwa na Manohantsoa kwa shuti la mbali lililomshinda kipa wa Morocco, El Mehdi Al Harrar .
Bao hilo liliwaamsha Morocco walioongeza kasi ya mshambulizi kwenye lango la Madagascar na kupata bao la kusawazisha dakika ya 27 lililofungwa na Mehri kwa kichwa baada ya kuinasa krosi ya Khalid Baba.
Ikiwa imebaki dakika moja kabla ya timu kwenda mapumziko, Morocco waliandika bao la pili lililofungwa na Lamlioui ambaye aliinasa krosi ya Mohamed Boulacsout, akautuliza vyema mpira na kuujaza wavuni.
Madagascar walikianza kipindi cha pili kwa utulivu na kupata bao la kusawazisha dakika ya 68 lililofungwa na Toky Rakotondraibe aliyetokea benchi akiutumia mpira ulioanzia kwa Manohantsoa.

Baada ya bao hilo kila timu ilicheza kwa kujihami na kushambulia kwa tahadhari lakini walikuwa Morocco waliokamilisha vyema hesabu zao kwa kuandika bao la tatu na la ushindi lililofungwa na Lamlioui ambaye amefikisha mabao sita kwenye CHAN 2024.
Lamlioui ambaye pia ndiye nyota wa mchezo huo, alifunga bao hilo kwa shuti la mbali huku kipa wa Madagascar, Ramandimbisoa akiwa mbali na eneo lake.
Katika mechi ya kuwania nafasi ya tatu iliyopigwa jana Ijumaa, Agosti 29, 2025, Senegal waliilaza Sudan 4-2 kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida.
Michuano ya CHAN 2024 iliyoanza kutimua vumbi Agosti 2, 2025 jijini Dar es Salaam, imefanyika katika nchi za Kenya, Uganda na Tanzania.
