Na mwandishi wetu
Wallace Karia amechaguliwa kwa mara nyingine kuendelea kuliongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumamosi hii, Agosti 16, 2025 mkoani Tanga.
Karia ameshinda nafasi hiyo kwa asilimia 100 akiwa mgombea pekee katika uchaguzi ambao ulipingwa Mahakama Kuu na jopo la mawakili lakini pingamizi hilo lilikwama na uchaguzi ukafanyika kama kawaida.
Mawakili hao walikuwa wakipinga hatua ya Karia kupendekezwa peke yake kugombea nafasi hiyo na kutaka mchakato wa uchaguzi ufanyike upya ili kiongozi huyo apate wapinzani.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Karia alisema safari ya kuelekea katika uchaguzi huo haikuwa nyepesi na kuifananisha na kitendo cha kukiweka chuma kwenye moto ili kiwe imara.
“Changamoto tuliyokutana nayo ni kama kutukumbusha kwamba tuna kazi mbele yetu na ni lazima tukabiliane nayo,” alisema Karia ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Karia pia alisema kitendo cha yeye kuchaguliwa kwa mara nyingine kisionekane kama ni ushindi binafsi bali ni sawa na kupewa jukumu la kuendelea kufanya maboresho katika kusimamia soka nchini Tanzania.
Mara baada ya ushindi huo, Karia kwa mujibu wa katiba ya TFF, alimpitisha Athuman Nyamlani kuwa makamu wa rais wa shirikisho hilo, wadhifa ambao alikuwa akiushikilia.
Kwa upande wa wajumbe sita wa kamati ya utendaji ya TFF waliopita katika nafasi hizo ni Khalid Mohamed, Hosseah Lugano, Issa Bukuku, Salum Kulunge, Mohamed Aden na James Mhagama.
Hii ni mara ya tatu kwa Karia kuchaguliwa kuliongoza shirikisho hilo, mara ya kwanza aliingia madarakani mwaka 2017 kabla ya kuchaguliwa mara ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2021.
