Na mwandishi wetu
Rais wa Kenya, William Ruto ameendelea kutoa motisha kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars ambao sasa amaehi kuwapa nyumba kila mmoja.
Wachezaji hao watapewa nyumba za nyumba ya vyumba viwili kila mmoja iwapo watafuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wandani (CHAN) inayoendelea nchini Kenya, Tanzania na Uganda.
Harambee ambayo ipo Kundi A hadi sasa imeshinda mechi mbili, sare moja na Jumapili itacheza mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Zambia.
Akizungumza na wachezaji hao Jumatatu hii Agosti 11, 2025 kwenye Hoteli ya Pullman mjini Nairobi, Rais Ruto pia aliahidi kumpa kila mchezaji Sh 2.5 milioni za Kenya iwapo wataifunga Zambia.
Ahadi ya Sh milioni 2.5 inakuwa motisha nyingine kubwa kwa wachezaji hao ambao awali aliwaahidi iwapo watashinda mechi yoyote atawapa Sh milioni moja ya Kenya kwa kila mchezaji.
Katika ahadi yake ya awali, mbali ya Sh milioni moja kwa kila mchezaji, Rais Ruto pia aliahidi kumpa kila mchezaji wa timu hiyo Sh 500,000 za Kenya kwa kila mechi ambayo watatoka sare.
Kuhusu ahadi ya nyumba, Rais Ruto ameahidi kuitekeleza kupitia mradi wa nyumba za bei nafuu ambao anaufanya nchini Kenya ambapo watakaonufaika katika ahadi hizo ni wachezaji wote 27 na viongozi 15 wa benchi la ufundi.
Taarifa ya nyongeza hiyo ya ahadi za Rais Ruto ilitolewa na msemaji wa Ikulu ya Kenya, Hussein Mohamed ambaye alisema wachezaji hao watajengewa nyumba kwenye maeneo ambayo watachagua wenyewe.
Ahadi za Rais Ruto kwa wachezaji wa Harambee zimeonekana kufurahiwa na wananchi wa Kenya hasa wapenda michezo ingawa wapinzani wake wa kisiasa wameanza kuhoji mantiki ya ahadi hizo.
Kimataifa Wachezaji Harambee kuzawadiwa nyumba
Wachezaji Harambee kuzawadiwa nyumba
Read also
