Na mwandishi wetu
Mabao ya Clement Mzize yameiwezesha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kutoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Madagascar katika mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Stars imeibuka na ushindi huo leo Jumamosi, Agosti 9, 2025 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na hivyo kufuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoendelea katika nchi za Tanzania, Uganda na Kenya.
Mzize ambaye pia ni mshambuliaji wa timu ya Yanga na ndiye aliyetajwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, aliandika bao la kwanza dakika ya 13, bao lililoanzia kwa mpira wa Iddi Suleiman Nado.
Mpira huo ulizua kizaazaa kwenye lango la Madagasrcar kabla ya kumkuta Mudathir Yahya ambaye shuti lake liligonga mwamba ndipo Mzize alipomalizia kwa kufunga goli.
Dakika saba baadaye, Mzize alindika bao la pili, safari hii akifunga kwa kumalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Feisal Salum au Fei Toto.
Madagascar walionesha utulivu licha ya kufungwa mabao hayo huku wakicheza pasi za uhakika na kuisumbua safu ya ulinzi ya Stars na juhudi zao kuzaa matunda kwa kupata bao pekee dakika ya 34 lililofungwa na Razafimahatana kwa pasi ya Rafanomezantsoa.
Stars hadi sasa haijapoteza hata mechi moja katika Kundi B, imeshashinda mechi zake za awali dhidi ya Burkina Faso, mabao 2-0 na dhidi ya Mauritania bao 1-0.
Timu hiyo imefikisha pointi tisa ikisubiri kumalizia mechi zake za makundi kwa kucheza na Afrika ya Kati, mechi itakayochezwa Jumamosi ijayo Agosti 16, 2025.
Kimataifa Mzize aipeleka Stars robo fainali CHAN
Mzize aipeleka Stars robo fainali CHAN
Read also
