Zimbwe Jr rasmi Yanga
Na mwandishi wetu
Hatimaye Yanga imekamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa siku nyingi wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ na kumaliza mjadala wa siku za karibuni kuhusu hatma ya mchezaji huyo.
Zimbwe ambaye amekuwa nahodha wa Simba kwa miaka kadhaa kuanzia mwaka 2017 akiwa nahodha msaidizi kabla ya baadaye kuwa nahodha mkuu hadi anaachana na timu hiyo.
Ameichezea Simba kwa takriban miaka 11 akiwa na namba ya uhakika kikosi cha kwanza na pia katika kipindi hicho amekuwa mchezaji tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Taarifa iliyopatikana leo Jumatano Agosti 6, 2025 imeeleza kuwa beki huyo wa kushoto ambaye pia anafahamika kwa jina la utani la Tshabalala, amesaini Yanga kwa mkataba wa miaka miwili.
Yanga imemsajili mchezaji huyo kutoka kwa mahasimu wao Simba, timu aliyoichezea kwa mafanikio na kuacha rekodi kadhaa za kuvutia ikiwamo kubeba mataji kadhaa ya ligi kuu Tanzania Bara.
Akiwa na Simba, Zimbwe pia ameiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu pamoja na kufikia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mara moja.
Kabla ya hapo, Simba ilifikia hatua ya fainali kwenye michuano ya klabu barani Afrika mwaka 1993.
Saa kadhaa baada ya Yanga kuweka wazi taarifa hizo, picha za mchezaji huyo akiwa amevaa jezi ya Yanga zilianza kutapakaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
Zimbwe alianza kuonesha makali yake akiwa na timu kadhaa za jijini Dar es Salaam kabla ya kujiunga na timu ya vijana ya Azam FC lakini hakuweza kutamba kabla ya kujiunga na Kagera Sugar.
Akiwa Kagera Sugar, mchezaji huyo alionesha umahiri wake katika nafasi ya beki wa kushoto na hatimaye kusajiliwa na Simba msimu wa 2014-15 na ingawa awali alipewa jina la utani la Tshabalala, mwenyewe anadaiwa kulipenda zaidi jina la utani la Zimbwe ambalo ni la beki wa zamani wa Yanga, Said Mwaibambe Zimbwe ambaye pia alifahamika kwa jina la utani la Terry Butcher, beki wa zamani wa England..
