Na mwandishi wetu
Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Mbwana Samatta amejiunga na timu ya Le Havre inayoshiriki Ligi Kuu Ufaransa maarufu Ligi 1.
Taarifa kutoka katika klabu hiyo zilieleza kuwa Samatta amesaini mkataba wa mwaka mmoja na anakuwa Mtanzania wa kwanza kucheza soka Ufaransa katika ligi hiyo ambayo ni moja ya ligi tano bora barani Ulaya.
Samatta, 32, ambaye pia anajulikana kwa jina la Samagoal kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao, amekabidhiwa jezi namba 70 katika timu hiyo.
Nyota huyo wa zamani wa Simba amesajiliwa na timu hiyo kutokana na uzoefu alionao na uwezo wake katika kuzifumania nyavu.
Baada ya kuonesha uwezo wake akiwa na kikosi cha Simba, Samatta alisajiliwa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo alizidi kuonesha umahiri wake katika ligi hiyo.
Akiwa na timu hiyo moja ya mafanikio makubwa aliyoyapata mbali na kubeba mataji kadhaa ya ligi kuu nchini humo, pia alifanikiwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015.
Katika kipindi hicho hicho, Samatta alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Afrika.
Baada ya hapo nyota ya mchezaji huyo ilianza kung’ara barani Ulaya ambapo alitimkia nchini Ubelgiji na kujiunga na klabu ya Genk na kuiwezesha kubeba taji la ligi kuu nchini humo.
Ubora wake baada ya hapo ulimuwezesha kusajiliwa kwa muda mfupi na klabu ya Aston Villa na hivyo kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza katika Ligi Kuu England, ligi nyingine kubwa barani Ulaya.
Baada ya Aston Villa, Samatta alizichezea Fenerbahçe ya Uturuki, Royal Antwerp ya Ubelgiji kabla ya kurudi Genk mara ya pili na kabla ya kusajiliwa Harve alikuwa akiichezea PAOK ya Ugiriki hadi mwishoni mwa msimu uliopita wa 2024-25.
Kimataifa Samatta ahamia Ligi Kuu Ufaransa
Samatta ahamia Ligi Kuu Ufaransa
Read also
