Nairobi, Kenya
Gavana wa zamani wa Nairobi, Mike Sonko ameahidi kutoa Sh 400 milioni za Kenya kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ iwapo watashinda taji la michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Zawadi hiyo inawafanya wachezaji wa Harambee Stars kupata jumla ya Sh bilioni 1 za Kenya baada ya Rais wa Kenya, William Ruto naye kuwaahidi Sh milioni 600 kama wakibeba taji hilo.
Sonko hata hivyo alisema kwamba ahadi aliyoitoa haina nia ya kushindana na Rais Ruto badala yake ni kumuunga mkono kiongozi huyo mkuu wa nchi.
“Rais amefanya jambo zuri la kuwahamasisha wachezaji, siko katika mashindano naye, nataka wabebe kombe na wakifanya hivyo nitawapa Sh milioni 400, vijana sasa mna bilioni 1,” alisema Sonko.
Sonko alisema kwamba bado anakumbuka siku za nyuma alivyokuwa akitoa ahadi kwa mchezaji mmoja mmoja anayeonesha juhudi badala yake anadhani jambo hilo si zuri kwani linaivunja moyo timu.
“Kuna siku nilikuwa natoa zawadi kwa wachezaji baada ya kufunga goli, lakini hilo kuna wakati linaleta ubinafsi kwenye timu, mchezaji anaweza akapoteza nafasi wakati angeweza kutoa pasi kwa mwingine ambaye yuko katika nafasi nzuri ya kufunga,” alisema Sonko.
Sonko pia aliwataka viongozi wengine nchini Kenya kuiunga mkono timu yao ya taifa kwa kutoa ahadi za kuwapa motisha wachezaji.
Wakati Sonko ameahidi kutoa Sh milioni 400 iwapo timu hiyo itabeba taji, Rais Ruto ahadi zake zinaanzia timu itakaposhinda Sh milioni moja kwa kila mchezaji, sare Sh milioni 500 na ahadi nyingine kuanzia robo fainali, nusu na fainali.
Michuano ya CHAN ambayo wenyeji wake ni nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, ilianza kutimua vumbi Agosti 2 jijini Dar es Salaam na Kenya tayari wametupa karata yao ya kwanza dhidi ya DR Congo na kutoka na ushindi wa bao 1-0 wakati Tanzania iliilaza Burkina Faso mabao 2-0.
