Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imeanza na mguu mzuri fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN 2024 kwa kuilaza Burkina Faso mabao 2-0.
Katika mechi hiyo ya ufunguzi ya Kundi B iliyopigwa Jumamosi hii Agosti 2, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Stars waliandika bao lao la kwanza dakika chache kabla ya mapumziko.
Bao hilo lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Abdul Suleiman ‘Sopu’ baada ya Frank Tologo wa Burkina Faso kumchezea ndivyo sivyo Clement Mzize akiwa ndani ya eneo la 18.
Stars waliandika bao la pili katika dakika ya 74 lililofungwa na Mohamed Hussein Zimbwe Jr, aliyekuwa beki na nahodha wa timu ya Simba ambayo ameachana nayo siku za karibuni.
Katika mechi hiyo, Stars walionesha kila dalili za kusaka ushindi kwa kuanza kulisakama lango la Burkina Faso, mapema dakika ya nne ya mchezo huo.
Katika shambulizi hilo, Clement Mzize aliufumania mpira akiwa wingi ya kulia na kuambaa nao kabla ya kufumua shuti lakini umakini wa kipa wa Burkina Faso, Ladji Sanou ulikuwa kikwazo.
Dakika nne baadaye, Stars walifanya shambulzii lingine na safari hii, Mudathir Yahya alimuunganishia pasi Feisal Salum ‘Fei Toto’ambaye alifumua shuti lakini kwa mara nyingine uimara wa kipa Sanou uliinyima Stars bao.
Burkina Faso nao katika dakika ya 18 walifanya shambulizi katika lango la Stars lakini shuti lililopigwa na Souleymane Sangare liliokolewa na kipa wa Stars, Yakoub Ali.
Stars ambao wapo Kundi B watacheza mechi ya pili Agosti 6 dhidi ya Mauritania kabla ya kucheza mechi ya tatu Agosti 9 dhidi ya Madagascar na kukamilisha mechi za kundi hilo Agosti 16 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kimataifa Stars yaanza CHAN na mguu mzuri
Stars yaanza CHAN na mguu mzuri
Read also
