Seoul, Korea Kusini
Nahodha wa klabu ya Tottenham Hotspur, Son Heung-min (pichani) amesema ataachana na timu hiyo akiwa ameweka rekodi ya kuichezea kwa mafanikio kwa kipindi cha miaka 10.
Son, mshambuliaji kutoka Korea Kusini alijiunga na Spurs mwaka 2015 akitokea Bayer Leverkusen ya Ujerumani na hadi sasa ameifungia mabao 173 katika mechi 454.
Alikuwa ndiye nahodha wa timu hiyo wakati ikiiadhibu Man United katika fainali ya Europa Ligi iliyopigwa Mei mwaka huu na hivyo kuiwezesha Spurs kubeba taji lao la kwanza baada ya miaka 17.
Son, 33, mkataba wake Spurs unafikia ukomo mwaka 2026 na kwa sasa anaendelea vizuri katika mazungumzo ya kujiunga na Los Angeles FC ya Marekani, timu inayoshiriki Ligi Kuu Marekani maarufu MLS.
Akizungumzia uamuzi huo akiwa karibu na kocha mpya wa Spurs, Thomas Frank, Son alisema katika maisha yake ya soka huo ni uamuzi mgumu mno ambao ameamua kuufanya.
“Nilikuja hapa London Kaskazini (Spurs) nikiwa mdogo, kijana mdogo tu sijui hata kuzungumza Kiingereza, kuondoka klabu hii nikiwa mtu mzima ni jambo la kujivunia sana,” alisema Son.
Spurs wapo katika jiji la Seoul nchini Korea Kusini katika ziara ya kujinoa kwa ajili ya msimu mpya wa 2025-26 ambapo Son anatarajia kuwa nahodha wakati timu hiyo ikiumana na Newcastle Jumapili hii.
Akimzungumzia Son, kocha Frank ambaye alikabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo Juni mwaka huu akichukua nafasi ya Ange Postecoglou, alimtaja Son kuwa ni mkongwe wa kweli wa Spurs na mmoja wa wachezaji bora waliocheza Ligi Kuu England.
