Manchester, England
Man United inadaiwa kuwa katika mpango wa kumuuza mshambuliaji wake, Rasmus Hojlund kwa ada inayotajwa kufikia Pauni 30 milioni.
Habari hizo zimekuja ikiwa ni siku chache tangu mshambuliaji huyo kutoka Denmark afunge mabao mawili katika mechi dhidi ya Bournemouth iliyopigwa Jumatano iliyopita mjini Chicago.
Mara baada ya mechi hiyo, waandishi walitaka kujua msimamo wa Hojlund baada ya habari kwamba Man United ina mpango wa kumsajili mshambuliaji Benjamin Sesko anayekipiga katika klabu ya RB Leipzig.
Mpango wa kumsajili Sesko mwenye umri wa miaka 22 ambaye pia anawindwa na Newcastle unatajwa kuwa sababu kubwa ambayo inaweza kutoa ushawishi kwa Man United kumpiga bei Hojlund.
Suala la kumuuza mshambuliaji huyo pia huenda likachangiwa na hoja ya kwamba Man United inataka kujiweka sawa katika kanuni za Ligi Kuu England zinazohusu faida.
Ikitokea Man United kumuuza mshambuliaji huyo kwa Pauni 30 milioni, itakuwa hasara kwa timu hiyo kwa kuwa thamani yake inatajwa kufikia Pauni 43 milioni, alisajiliwa Man United kwa mkataba wa miaka mitano akiwa ameitumikia miwili hadi sasa.
Tangu kufunguliwa kwa dirisha la usajili wa Majira ya Kiangazi, Man United imetumia Pauni 130 kusajili wachezaji wawili ambao ni Bryan Mbeumo na matheus Cunha.
Hojlund alisajiliwa na Man United wakati wa kocha Erik ten Hag na ingawa kulikuwa na matumaini makubwa lakini hadi sasa bado hajaonesha kile kilichotarajiwa na wengi.
Kimataifa Man Utd kumpiga bei Hojlund
Man Utd kumpiga bei Hojlund
Read also
