Fenerbahce, Uturuki
Kocha Jose Mourinho ameweka wazi kuhusu shauku yake ya kutaka kuwa kocha wa timu ya taifa lake la Ureno wakati akiwa kwenye ubora wake.
Mourinho, 62, kwa sasa anainoa klabu ya Fenerbahce ya nchini Uturuki na amebakiwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na timu hiyo.
Mourinho aliondoka nchini Ureno mwaka 2004 baada ya kuiwezesha FC Porto kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kujiunga na Chelsea ambapo alianza kupata umaarufu hadi kubatizwa jina la utani la Special One.
Mbali na Chelsea na FC Porto, Mourinho pia amewahi kuzinoa timu za Tottenham, Inter Milan, Man United, Real Madrid na AS Roma na hadi sasa ana rekodi ya kubeba mataji 26 akiwa kocha wa timu alizopita.
Mourinho hata hivyo alipoulizwa kama angependa kuendelea kuwa kocha wa klabu au timu ya taifa, alisema lolote kwake sawa lakini hakuficha shauku yake ya kurudi Ureno.
“Ni hakika nitarudi Ureno, hilo halijatokea na si kwa sababu naelekea mwisho wa kazi ya ukocha, hapana huko bado ni mbali sana, sitaki kurudi Ureno kama mstaafu au katika miaka yangu ya mwisho ya kazi,” alisema Mourinho.
Mourinho aliongeza kuwa angependa arudi Ureno akiwa katika ubora wake, akiwa mwenye afya nzuri kimwili na kiakili na mwenye nguvu na kusisitiza kuwa ni lazima arudi.
Mourinho hata hivyo aliwahi kukanusha habari kwamba alifanya mazungumzo na viongozi wa Shirikisho la Soka Ureno ili awe kocha wa timu hiyo kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia 2026 ingawa pia aliwahi kusema kwamba alikataa mara mbili nafasi ya kuwa kocha wa timu ya Ureno.
