New Jersey, Marekani
Chelsea imefanikiwa kubeba taji la michuano ya Fifa ya Klabu ya Dunia baada ya kuilaza PSG mabao 3-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa Jumapili hii Julai 13, 2025.
Ushindi wa Chelsea ni tukio ambalo halikutarajiwa kwani timu hiyo haikuwa kati ya timu zilizopewa nafasi ya kubeba taji la michuano hiyo iliyoshirikisha timu kadhaa kubwa zikiwamo, Real Madrid na Bayern Munich.
Shujaa wa Chelsea katika mechi hiyo alikuwa ni kiungo Cole Palmer ambaye alifunga mabao mawili dakika za 22 na 30 kabla ya kuwa mpishi wa bao la tatu lililofungwa na Joao Pedro dakika chache kabla ya timu kwenda mapumziko.
PSG ndiyo iliyopewa nafasi kubwa ya kubeba taji hilo hasa baada ya kubeba taji la Ligi 1 ya Ufaransa na Ligi ya Mabingwa Ulaya na matarajio yaliyokuwa kwa timu hiyo kubeba taji la tatu.
Matumaini ya PSG chini ya kocha Luis Enrique hata hivyo yalizimwa na Chelsea ambao sasa wameweka historia ya kubeba taji hilo katika michuano ambayo inafanyika mara ya kwanza katika mfumo mpya unaoshirikisha timu nyingi.
Katika mechi hiyo, kocha wa Chelsea, Enzo Maresca alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili katika kikosi kilichocheza nusu fainali, akiwapa nafasi Levi Colwill na Reece James badala ya Tosin Adarabioyo na Christopher Nkunku.
Mabadiliko hayo yaliipa faida timu hiyo ambayo ilionekana kuwa tishio zaidi huku Palmer akionesha mapema alivyopania kuipa ushindi timu yake katika dakika ya saba baada ya mpira alioupiga kwa mguu wa kushoto kutoka nje.
PSG nao walianza kuja juu baada ya kushtuliwa na kama si umahiri wa beki Marc Cucurella kuzuia pasi hatari iliyopigwa na Desire Doue kwenda kwa Achraf Hakimi mambo yangekuwa mabaya kwa Chelsea.
“Tunajisikia vizuri, kocha alikuja na mpango mzuri, alijua wapi kulikuwa na nafasi na alijitahidi kunifanya niwe huru kadri ilivyowezekana, nami nikamjibu kwa kufunga mabao,” alisema Palmer.
Naye kocha Maresca alisema kwamba hana la kusema zaidi kwa wachezaji wake na kilichotokea ni kwamba walishinda mechi hiyo katika dakika kumi za kwanza na walijua jinsi walivyotaka kucheza.
Mechi hiyo ya fainali ilihudhuriwa na Rais wa Marekenia, Donald Trump ambaye ndiye aliyewakabidhi Chelsea taji hilo na alitajwa kama mgeni wa Rais wa Fifa, Gianni Infantino.
Fainali za michuano hiyo ya Fifa zimekamilika nchini Marekani kukiwa na malalamiko ya baadhi ya klabu kutaka zifutwe kwa kuwa zinavuruga ratiba za soka na kuwachosha wachezaji huku mechi zake zikishindwa kuvutia mashabiki wengi.
