New Jersey, Marekani
Kipa wa Real Madrid, Thibaut Courtois (pichani) ametaka mamlaka za usimamizi wa Ligi Kuu Hispania au La Liga kukubali maombi ya timu hiyo kutaka siku ya kuanza msimu mpya isogezwe mbele ili wachezaji wapate muda zaidi kupumzika.
Madrid ambao wametoka kutolewa kwenye michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu baada ya kulala kwa mabao 4-0 mbele ya PSG katika mechi ya nusu fainali, watauanza msimu mpya wa La Liga Agosti 19 kwa kuumana na Osasuna kwenye Uwanja wa Santiano Bernabeu.
Akizungumza mara baada ya kutolewa kwenye michuano hiyo ya Fifa, Courtois alisema ni matumaini yake kwamba La Liga wanaweza kubadili mechi au hata kuisogeza mbele na kuwa wiki inayofuata kwani kupumzika na kujiandaa ni muhimu kwa ligi na afya za wachezaji.
Hivi karibuni Real Madrid waliomba mechi za msimu mpya wa La Liga wa 2025-26 zichelewe kuanza wazo lililoungwa mkono na Umoja wa Wachezaji Hispania (AFE) ambao waliwasilisha ombi hilo kwa barua kwenda La Liga na Shirikisho la Soka Hispania.
Osasuna na Real Madrid wote hivi karibuni walikumbushia ombi hilo wakisisitiza umuhimu wa kupumzika na kujiandaa kwa msimu mpya kuwa ni jambo zuri kwa afya za wachezaji.
Kama ilivyo kwa klabu nyingine, Real Madrid nao baada ya kumaliza mashindano makubwa, wanahitaji wiki sita, wiki tatu kwa ajili ya mapumziko na wiki nyingine tatu za mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.
Tangu kuanzishwa kwa mashindano ya Klabu ya Dunia kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wachezaji na wasimamizi wa ligi akiwamo Rais wa La Liga, Javier Tebas ambaye ametaka mashindano hayo ya Fifa yafutwe kwani yanaharibu mifumo ya ligi za taifa hasa barani Ulaya.
Kimataifa Courtois aomba muda wa kupumzika
Courtois aomba muda wa kupumzika
Read also
