Na mwamdishi wetu
Miaka michache iliyopita wakati Yanga ikiwa katika harakati za kumsajili, Stephane Aziz Ki, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu usajili wa mchezaji huyo.
Yanga walishajiaminisha na kuuaminisha umma kwamba walishakamilisha usajili wa mchezaji huyo kutoka Burkina Faso lakini mwandishi mmoja wa habari akapinga na kudai kuwa Yanga walikuwa hawajakamilisha usajili huo.
Mjadala ule ulipamba moto, kila mmoja akishikilia msimamo wake lakini wakati mwandishi akitaka ushahidi, Yanga waliikwepa hoja hiyo na kushikilia msimamo kwamba kila kitu tayari.
Kwenye mitandao ya kijamii nako hali ikawa hivyo, msimamo wa wengi ukawa wa kuiunga mkono Yanga kwamba tayari ilikuwa imemsajili mchezaji huyo lakini swali la ushahidi wa kimaandishi au wowote lilikwepwa.
Ilikuwa kama vile hoja ya msingi inakimbiwa, hoja isiyo na ushahidi inashikiliwa na kuonekana ndio sahihi na mwandishi aliyetaka umma uoneshwe ushahidi hakuwa sahihi.
Mjadala uliendelea kupamba moto kwa siku kadhaa, kila upande ukishikilia lake, wakati yote hayo yakiendelea mchezaji mlengwa hakutambulishwa na ushahidi wa kimaandishi wa kumsajili haukuwekwa hadharani.
Baadaye, mchezaji akatambulishwa rasmi na mwandishi aliyekuwa akiwapinga naye akaibuka na kukiri kwamba hatimaye Yanga walikamilisha usajili.
Nini kilifuata baada ya hapo, mwandishi aliyepinga alionekana kama kushambuliwa na kuonekana muongo, haipendi Yanga.
Sakata zima la usajili ule lilinifundisha jambo moja, uandishi wa habari za michezo hasa kwenye mitandao ya kijamii umekosa weledi wa kitaaluma.
Katika taratibu za usajili kwenye vyombo vya habari kuna tetesi au mazungumzo ya awali, yote hayo yanaamisha kwamba usajili bado haujakamilika.
Kwa Aziz Ki, Yanga walikuwa katika mazungumzo, usajili wake ulikamilika baadaye hivyo mwandishi aliyesema kwamba Yanga walikuwa hawajakamilisha usajili alikuwa sahihi na ndicho kilichotakiwa kuelezwa kwenye vyombo vya habari.
Katika mazungumzo kuna kufikia muafa au kutofikia muafaka, hivyo kusema mchezaji amesajiliwa au amemalizana na klabu wakati mazungumzo yanaendelea si sahihi hata kidogo.
Ni sawa sawa na tetesi, zitabaki kuwa tetesi na wakati wa usajili ni vigumu kuzikwepa kwa sababu wakati mwingine zinatengenezwa na mawakala au hata wachezaji wenyewe kutaka kujiuza.
Kuna tetesi ambazo mwisho wake zinakuwa kweli na tetesi nyingine zinaishia hivyo hivyo kwa suala la usajili kutokamilika.
Kwa Aziz Ki kilichokuwa ni kwamba mazungumzo yalikuwa yakiendelea na ndio maana mwandishi yule alikuwa sahihi kusema kwamba kwa wakati huo haikuwa sahihi kwa Yanga kutamba kwamba Aziz Ki ni mchezaji wao.
Kwa hiyo ni vizuri kuepuka kuzihusisha tetesi na mazungumzo ya awali na kukamilika kwa usajili wa mchezaji au kocha.
Mifano ni mingi, mmojawapo ni wa aliyekuwa kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti kukabidhiwa jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Brazil, kwanza ilikuwa tetesi, habari ya pili ikawa mazungumzo yameanza na yanakwenda vizuri na mwisho kocha akatangazwa rasmi.
Ni hivyo hivyo kwa Lionel Messi ambaye kabla ya kusajiliwa Inter Miami ya Marekani zilikuwapo tetesi za kutakiwa Saudi Arabia, kurudi Barcelona na hapo hapo kukawa na mazungumzo yanaendelea pande zote na mwishowe Messi akasaini Inter Miami.
Kwa Aziz Ki, ni kama vile hadithi yake ya mwanzo kujiunga na Yanga haikutosha, hivi karibuni tena ikaibuka hadithi nyingine yenye sifa za upotoshaji ikidai kwamba Wydad ya Morocco hawamtaki mchezaji huyo na anarudi Yanga.
Habari hii ilivuka mipaka, ilianza kama tetesi lakini siku baada ya siku baadhi ya watu wakajitahidi kuuaminisha umma kuwa ni habari sahihi kwa namna ilivyokuwa ikiandikwa ingawa haikuwa na dalili za ukweli na mwisho wa siku ikabanika kwamba ni uwongo.
KWa hiyo yote hayo yatoshe kuwafanya waandishi kutofautisha tetesi za usajili na kukamilika kwa usajili au mazungumzo ya awali na kukamilika kwa usajili, usajili unakamilika baada ya makubaliano si mazungumzo ya awali.
Soka Uandishi wa habari katika usajili wa Aziz Ki
Uandishi wa habari katika usajili wa Aziz Ki
Read also
