Na mwandishi wetu
Kwa mara ya kwanza mechi ya watani wa jadi katika soka la Tanzania, Simba na Yanga ilichezeshwa na mwamuzi Amin Mohammed Omar kutoka nchini Misri.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Juni 25, 2025 na Yanga kutoka na ushindi wa mabao 2-0, bila shaka hakukuwa na matukio yaliyoacha maswali au kuzua mijadala kuhusu ubora wa mwamuzi.
Ukiachana na tukio la kipa wa Simba, Mousa Camara kugongana na kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua na kuzaa penalti iliyozaa bao, hakuna tukio jingine lililozua mijadala, mechi ilikwenda vizuri na kwa utulivu wa hali ya juu.
Mjadala wa tukio la Pacome na Camara, kwa Simba wanaamini haikuwa penalti kwa kuwa kipa aliruka kuufuata mpira wakati Yanga wanaamini ilikuwa penalti kutokana na mgongano uliochangiwa kwa kiasi kikubwa na mruko wa kipa.
Nje ya tukio hilo, mwenendo wa mchezo na jinsi mwamuzi alivyokuwa uwanjani kila eneo na kufuatilia kwa umakini ni kati ya mambo ambayo yameacha somo kwa waamuzi wa Tanzania.
Ukiachana na umakini huo, mwamuzi huyo pia alituonesha namna mwamuzi anavyotakiwa kuutawala mchezo kwa kutokubali kuchezewa au kujaribiwa na wachezaji pale anapoamini kwamba amefanya uamuzi sahihi.
Mfano hakukubali mchezaji kuonesha kwa ishara ya kutoridhika na maamuzi anayoyachukua kwa kujifanya ameonewa au kufanya tukio lolote baada ya filimbi kupulizwa.
Mifano ya hiyo ilijionesha kwa Kibu Denis wa Simba pale mwamuzi alipopuliza filimbi kuashiria mpira umetoka na urushwe kuelekea lango la Simba.
Kibu pengine kwa kutaka kumjaribu, akaonesha kuchukizwa na maamuzi hayo kwa kuudunda mpira chini kwa hasira ili ionekane kama Simba ndio waliotakiwa kurusha mpira huo kuelekea kwa Yanga.
Mwamuzi alimfuata kwa karibu Kibu huku akionekana mwenye hasira na kumuonya kwa ishara ya kukataa kujaribiwa.
Tukio kama hilo pia lilitokea kwa Duke Abuya wa Yanga aliyeanguka chini kama vile aliyechezewa rafu mbaya na kutaka kumshawishi mwamuzi apulize filimbi lakini mwamuzi huyo alimtolea macho na kumpa ishara ya kutotaka kujaribiwa.
Tukio kama hilo linanikumbusa kisa alichowahi kusimulia mchezaji wa zamani wa timu ya Liverpool ya England, Steven Gerard wakati akimsifia mwamuzi Pierluigi Collina wa Italia kwa umakini.
Katika moja ya mechi, Steven Gerard akiwa nahodha Liverpool alijaribu kwa uwongo kujifanya kaumizwa ili kumshawishi mwamuzi apulize filimbi kuibeba timu yake lakini mwamuzi huyo alibaini tukio hilo na kumtolea macho ya ukali huku akimwambia ‘stop fuck around with me’ (acha kuniletea mzaha, au acha kunijaribu).
Kitu hicho pia ndicho nilichokiona kwa Amin Mohammed Omar, hakuruhusu wachezaji wafanye mzaha na kazi yake au wamjaribu.
Clement Mzize wa Yanga aliubutua mpira nje wakati mwamuzi alishapuliza filimbi, Shadrack Boka naye hivyo hivyo alipiga mpira kwa lengo la kufunga goli baada ya mwamuzi kupuliza filimbi kuashiria kuotea.
Katika matukio yote hayo mawili, Amin Mohammed Omar alionesha jinsi asivyotaka masihara kazini, wote akawaonya kwa ishara ya ukali.
Kuyasimamia matukio hayo kama alivyofanya Amin Mohammed Omar ni sababu tosha inayosaidia kulinda hadhi na heshima ya mwamuzi kwa kutokubali kuchezewa, hiyo ni mbali na umakini ambalo ni jambo la lazima kwa mwamuzi yeyote.
Kwa hiyo ni vyema kwa waamuzi wetu mbali na somo la umakini lakini wawapo uwanjani wasikubali kuchezewa au kujaribiwa na wachezaji.
Makala Mwamuzi Dar Derby kawaachia somo waamuzi Tanzania
Mwamuzi Dar Derby kawaachia somo waamuzi Tanzania
Read also
