Paris, Ufaransa
Uamuzi wa kuishusha daraja Olympique Lyon ya Ufaransa umefutwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Fedha kwa Klabu za soka Ufaransa (DNCG) na sasa timu hiyo itaendelea kucheza Ligi 1 badala ya Ligi 2.
DNCG hivi karibuni walitangaza kuishusha Lyon hadi Ligi 2 baada ya kubaini kuwapo na mwenendo usiofaa wa kifedha katika klabu hiyo ambayo imewahi kutwaa taji la Ligi 1 mara saba.
Uamuzi wa DNCG uliacha maswali mengi kwa mashabiki wa soka wa ndani na nje ya Ufaransa kutokana na hadhi ya klabu hiyo, uamuzi ambao pamoja na mambo mengine ya kifedha pia ulichangiwa na klabu hiyo kuwa na deni linalofikia Euro 175 milioni
Mapema wiki hii, taarifa ya klabu ya Lyon ilieleza kuwa rufaa waliyokata imekubaliwa na DNCG baada ya kuwasilisha mpango wao mpya wa fedha ulioonekana unatosha kuiruhusu klabu hiyo kuendelea kushiriki Ligi 1.
Kwa uamuzi huo wa DNCG maana yake ni kwamba Lyon sasa wanaweza kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi 1 wa 2025-26 ambao unatarajia kuanza rasmi Agosti mwaka huu.
Mabadiliko ya uongozi na mfumo wa klabu ya Lyon ndiyo yanayotajwa kuishawishi DNCG kuamini kwamba klabu hiyo sasa ipo katika mwelekeo mpya.
Uamuzi wa kuirudisha Lyon Ligi 1 si tu kwamba unairudisha klabu hiyo katika hadhi yake lakini pia unadumisha na kuendeleza ushindani na ushabiki katika ligi hiyo ambayo ni moja ya ligi kubwa za soka Ulaya na duniani.
Kimataifa Lyon yafutiwa adhabu ya kushushwa daraja
Lyon yafutiwa adhabu ya kushushwa daraja
Read also
