Na Hassan Kingu
Msimu wa 2024-25 umeisha, naiangalia Simba iliyofikia fainali Kombe la Shirikisho Afrika, ikafungwa na RS Berkane mabao 2-0 na kushindwa kubeba taji la michuano hiyo.
Simba hiyo hiyo, iliyoishia nafasi ya pili Ligi Kuu NBC na kufungwa mabao 2-0 na Yanga, mashabiki wanaamini timu yao imefeli na tatizo ni mwenyekiti wao, Murtaza Mangungu.
Ndoto na matumaini ya Simba kubeba taji hilo ziliyeyuka kama ambavyo ziliyeyuka ndoto za kubeba taji la Ligi Kuu NBC ambalo liliishia mikononi mwa mahasimu wao Yanga.
Kama hiyo haitoshi, mahasimu wao Yanga wakaendelea kuwapa vipigo kwa mara ya tano mfululizo huku wakilibeba taji la ligi hiyo kwa mara ya nne mfululizo.
Simba ambayo imefikia fainali Kombe la Shirikisho Afrika haikuambulia hata taji moja katika msimu wa 2024-25 huku ni kufeli na wenyewe wanaaminishana kwamba aliyewafelisha ni Mangungu.
Nyimbo za hatumtaki Mangungu zimesikika kwenye mitandao ya kijamii na ukizisikiliza nyimbo hizo unaweza kujiaminisha moja kwa moja kuwa Simba haina tatizo jingine isipokuwa Mangungu. Huu ni uwongo wa wazi.
Kwa mtu asiyefahamu kuhusu Mangungu pia anaweza kudhani kwamba Mangungu ndiye kocha wa timu au ndiye ofisa mtendaji mkuu yaani CEO, kumbe sivyo Mangungu ni mwenyekiti wa klabu.
Mara ya mwisho Simba kufikia hatua ya fainali kwenye michuano ya klabu barani Afrika inayoandaliwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ilikuwa mwaka 1993, miaka takriban 31 iliyopita, tulidhani kwamba kufikia hatua hiyo msimu huu ni mafanikio, hapana ni kufeli na sababu ni Mangungu.
Kwa kilichotokea katika Simba msimu huu baadhi yetu tunaamini tatizo si Mangungu bali tatizo ni lile lile, mafanikio ya Yanga na vipigo mara nne mfululizo.
Klabu hizi mbili zina tabia ya kuteswa na mafanikio ya mmoja wao kiasi cha kujinyima hata kufurahia mafanikio mengine ya kihistoria waliyofikia.

Kuhusu Mangungu ni ama wanachama wamejazwa na maadui zake mitazamo ya kuamini kuwa yeye ndiye tatizo, iwe ni kwa kulipwa au kutolipwa au hawajatafakari kwa kina wanachokizungumza kuhusu kiongozi huyo.
Inawezekana kuna watu wenye nguvu ndani ya Simba ambao hawamtaki Mangungu kwa hiyo hatua iliyofikia Simba katika msimu wa 2024-25 inageuzwa kuwa ni kufeli, tena kufeli kubaya na eneo sahihi la kumshughulikia Mangungu ni hilo.
Si vibaya kusema kwamba Simba imefeli hasa kwa kuwa haijapata taji lakini si sahihi kugeuza nongwa kufeli kwa aina ya msimu huu na kuuaminisha umma uamini kwamba tatizo alikuwa ni Mangungu.
Mtazamo wa Simba kufeli unaweza kuzungumziwa katika kukosa mataji, kufungwa na Yanga lakini huu hauwezi kuwa msimu wa hovyo kwa Simba badala yake unaweza kutajwa kuwa ni msimu ambao Simba imeteleza.
Katika kuteleza huko ni vyema kuangalia matatizo kwa mapana yake badala ya kumuangalia Mangungu na kujiaminisha kwamba ndiye tatizo na labda akiondoka mambo yatakuwa salama, huku ni kumpa Mangungu sifa ambazo hana.
Klabu yenye kocha, CEO, bodi na viongozi wengine lukuki wanaohusika moja kwa moja na maendeleo ya timu, hao wote hawana tatizo isipokuwa mwenye tatizo ni Mangungu pekee, bila shaka atakuwa na nguvu ya kipekee na anaogopwa.
Wakati Simba inasonga mbele hatua moja hadi nyingine kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, mashabiki walikuwa wakijivunia na hakuna aliyewahi kusema kwamba Mangungu ana msaada au amechangia kufikisha Simba ilipofikia.
Ni kama vile Mangungu alikuwa anasubiriwa Simba ishindwe, tena bila kujali imeshindwaje na katika hatua ipi ndipo waanze kumshutumu kwamba hatakiwi na ndiye tatizo.
Badala ya kuhangaika na Mangungu pekee, Simba waanze mipango ya kuboresha kikosi, warekebishe mapungufu yaliyowafanya wafike fainali na wasichukue taji la Shirikisho Afrika, wahakikishe wanakuwa na kikosi kipana kama cha Yanga.
Kama kuna kitu Simba wanatakiwa kujifunza kwa Yanga basi ni kuhakikisha wanakuwa na kikosi kipana na cha ushindani.
Baada ya hapo wasichoke, waendelee kujiuliza, baada ya kushika nafasi ya pili kwenye ligi, msimu ujao watawezaje kubeba taji na kama kuifunga Yanga kwao ndio kila kitu pia waweke mkakati huo.
Huyu Mangungu kama kweli wamemchoka na ndiye tatizo basi wasubiri kumtoa kwenye uchaguzi, mambo ya kupinduana kwa sasa hayana nafasi au yamepitwa na wakati.
