Na Hassan Kingu
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Kenya, Boniface Ambani (pichani) amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa AFC Leopards, klabu kongwe na maarufu ya soka Kenya na Afrika Mashariki na Kati.
Katika uchaguzi uliofanyika Juni 30, 2025, Ambani aliibuka mshindi na kukabidhiwa kiti kilichokuwa kikishikiliwa na Dan Shikanda kwa kupata kura 1,100 na kumshinda Vincent Mutokah aliyepata kura 681.
Ukiizungumzia Leopards unaitaja moja ya klabu kongwe nchini Kenya ambayo imekuwa na uhasama wa muda mrefu na Gor Mahia pia ya nchini humo.
Uhasama wa timu hizi mbili kwa Kenya ni sawa na Yanga na Simba kwa Tanzania au Man United na Man City kwa England, uhasama wao kwenye soka ni wa miaka mingi.
Kwa Leopards au Ingwe na Gor Mahia au K’ogalo, uhasama wao katika soka umebatizwa jina la Mashemeji Derby ni kama kwa hapa Tanzania tulivyo na Dar au Kariakoo Derby kwa Simba na Yanga.
Tofauti na hali ya uhasama ilivyo kwa Dar Derby, nchini Kenya kidogo mambo si mazuri kwa Mashemeji Derby kwa upande wa Leopards, hadhi na heshima ya timu hiyo imeshuka kwa muda mrefu sasa.
Ukweli kwamba Leopards ni kati ya timu zenye rekodi ya kuvutia katika Ligi Kuu Kenya kwa kutwaa taji la ligi hiyo mara 12 bado haufuti ukweli mwingine kwamba hadhi na heshima ya timu hiyo imekuwa chini kwa muda mrefu sasa.
Wakati Leopards wakibeba taji hilo mara 12, mahasimu wao Gor rekodi inaonesha wamebeba taji hilo mara 18 lakini kwa Leopards mara ya mwisho kubeba taji hilo ilikuwa mwaka 1998, kipindi ambacho kocha Mtazania, Sunday Kayuni alikuwa akiinoa timu hiyo.
Tangu hapo Leopards imekuwa ikiziangalia Gor na timu nyingine zikibeba taji hilo kuanzia timu za Ulinzi, Tusker, Oserian Fastac, Mathare United, Sofapaka na POlisi FC.
Si hivyo tu, Leopards pia ilifikia hadi hatua ya kushuka daraja hivyo kuzidi kupoteza hadhi yake kwenye soka la Kenya kabla ya kupambana na kurudi kwa mara nyingine.
Katika mazingira kama hayo, Ambani, mchezaji wa zamani wa timu hiyo na ambaye pia amewahi kucheza soka India na Oman, ana kibarua kuhakikisha hadhi na heshima ya Leopards inarudi katika soka la Kenya na Afrika Mashariki na Kati.
Kazi ya kwanza ni kuhakikisha timu hiyo inabeba taji la ligi kuu na kurudi kwenye michuano ya klabu Afrika na si tu kurudi kama mshiriki bali kurudi kama mshindani kama ilivyokuwa enzi za kina JJ Masiga na wenzake.
Kazi mojawapo kubwa inayomsubiri Ambani ni kuhakikisha timu hiyo inapata ufadhili wa nguvu ambao utamuwezesha kusajili wachezaji wa viwango vya juu.
Katika hilo tayari ana mtaji wa mashabiki kwani Leopards ni kati ya timu zenye mashabiki wengi Kenya lakini mtaji wake wa pili ni nguvu ya wanasiasa katika timu hiyo.
Mmoja wa wanasiasa ambaye anafahamika kwa miaka mingi kuwa shabiki kindakindaki wa Leopards ni Waziri Mkuu Kiongozi wa Kenya na kiongozi wa chama cha siasa cha ANC, Musalia Mudavadi.
Kwa Mudavadi, historia yake na Leopards ni ya kipekee kwani inaanzia kwa baba yake Moses Mudavad ambaye pia alikuwa shabiki na mfadhili wa timu hiyo, huu unaweza kuwa mtaji muhimu wa kwanza kwa Ambani.
Wanasiasa wengine ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuiunga mkono timu hiyo ni Alfred Sambu ambaye pia amewahi kuwa kiongozi, Edwin Sifuna, Ken Lusaka na wengineo.
Makundi hayo mawili ya wanasiasa na mashabiki yanaweza kuwa mtaji mzuri kwa Ambani pamoja na uzoefu wake katka kuhakikisha hadhi na heshima ya Leopards Afrika Mashariki na Kati inarudi kama zamani.
Ambani pia amekuwa mchambuzi wa soka kwa hiyo kuchaguliwa kwake kuiongoza Leopards kwake ni fursa muhimu ya kuyafanyia kazi baadhi ya mambo ambayo amekuwa akiyashauri kupitia vyanzo mbalimbali vya habari.
Kimataifa Ambani ataweza kuirudisha hadhi ya Leopards?
Ambani ataweza kuirudisha hadhi ya Leopards?
Related posts
Read also
