Monaco, Ufaransa
Kiungo wa zamani wa Man United Paul Pogba hatimaye amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya Monaco ya Ufaransa katika tukio lililomfanya amwage chozi la furaha.
Pogba, 32, aliyekuwa akitumikia adhabu baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu, sasa ni dhahiri anarudi kwenye soka la ushindani tangu asimame mwanzoni mwa msimu wa 2023-24.
Mara baada ya kusaini mkataba huo, Pogba huku akitokwa machozi na hapo hapo akionekana mwenye furaha alinukuliwa akisema,. ‘asante kwa ukweli’.
Pogba ambaye alikuwa na timu ya Ufaransa iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 2018, Novemba mwaka jana alifikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake na klabu ya Juventus na hivyo kuwa mchezaji huru tangu Machi mwaka huu.
Na ingawa Pogba ni Mfaransa lakini baada ya kusaini mkataba na Monaco sasa atapata fursa ya kucheza soka katika Ligi Kuu Ufaransa maarufu Ligi 1 kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka.
Pogba alianza kuonesha ubora wake Man United kabla ya kutimkia Juventus ambako alibeba mataji ya Serie A mara nne kabla ya kurudi tena Man United mwaka 2016 kwa ada ya Pauni 89 milioni ambapo alishinda mataji ya Europa na FA.
Kwa upande wa timu ya taifa ya Ufaransa, ameichezea timu hiyo mara 91 na ndiye mfungaji wa bao la mwisho wakati Ufaransa ikiibwaga Croatia 4-2 katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2018 na kubeba taji hilo.
Katika misimu yake mitatu ya mwisho akiwa Man United, Pogba aliandamwa na janga la kuwa majeruhi mara wa mara na kushindwa kutamba kabla ya kutimkia Juventus alipokumbana na kadhia ya madawa ya kuongeza nguvu na kupewa adhabu ya miaka minne ambayo baadaye ilipunguzwa.
Kimataifa Pogba amwaga chozi akisaini Monaco
Pogba amwaga chozi akisaini Monaco
Read also
