Florida, Marekani
Aliyekuwa kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema anaamini wazo la kuanzishwa michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu inayoshirikisha timu nyingi ni la hovyo.
Klopp mara kwa mara amekuwa akilalamikia kuhusu ratiba za msimu mmoja zinavyokuwa na mzigo wa mechi nyingi na jinsi mechi hizo zinavyochosha wachezaji.
Siku kadhaa kabla ya kuanza kwa michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu, Umoja wa Wanasoka Profesheno ulitioa ripoti na kusema kwamba wachezaji wanahitaji walau kuwa na wiki nne za mapumziko katika msimu mmoja.
Mwaka huu kwa mara ya kwanza michuano hiyo inayosimamiwa na Fifa imeshirikisha timu 32 na inahusisha mechi 48 ambapo timu ya Salzburg Red Bull, moja ya timu ambazo Klopp ni kiongozi tayari imetolewa katika hatua ya makundi.
Akizungumzia ubaya wa michuano hiyo, Klopp alisema kinachoangaliwa ni mechi tu na si mazingira ya matukio husika na ndio maana anaamini michuano hiyo ni wazo la hovyo kuwahi kufanywa katika soka.
“Watu ambao hata mara moja hawajawahi kuwa na kitu cha kufanya katika shughuli za kila siku ndio wanaokuja na mawazo yao, kuna ukichaa wa pesa katika ushiriki lakini pia si kwa kila timu,” alisema Klopp.
Akifafanua zaidi Klopp alisema mwaka jana kulikuwa na Copa America na michuano ya Ulaya na mwaka huu ni Kombe la Dunia la Klabu na mwakani ni Kombe la Dunia.
Klopp anaamini kuwapo kwa ratiba ya aina hiyo maana yake ni kwamba kwa wachezaji hakuna kupumzika kimwili na hata kiakili.
