Na mwandishi wetu
Baada ya Simba kufungwa na Yanga mabao 2-0 na kushindwa kubeba taji la Ligi Kuu NBC msimu wa 2024-25, meneja habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally ameibuka akiwashangaa wanaodai timu hiyo imefeli.
Baada ya Simba kushindwa kutamba mbele ya Yanga katika mechi hiyo ya mwisho ya ligi hiyo, mashabiki wa Simba wamekuwa wakisimangwa na wenzao wa Yanga hasa mitandaoni hoja mojawapo kuu ikiwa ni kufeli kwa timu hiyo.
Katika taarifa yake kwenye vyanzo mbalimbali Ally, amewataka wana Simba kuepuka presha za mitandaoni za watu anaodai wanaouaminisha umma kuwa timu hiyo imefeli kupita kiasi.
Akitetea alichokiita mafanikio, Ally alisema timu hiyo haijafeli bali imepiga hatua kubwa msimu huu kulinganisha na miaka ya nyuma na hilo ndilo lililokuwa lengo lao la kutengeneza timu ya ushindani.
Alifafanua kwamba msimu huu Simba imefanikiwa kucheza fainali ya CAF (Shirikisho Afrika), jambo ambalo limewashinda kwa takriban miaka 31 sasa.
Mara ya mwisho Simba kucheza hatua ya fainali ya michuano inayoandaliwa na CAF ni mwaka 1993 ilipocheza dhidi ya Stella ya Ivory Coast na kushindwa kutamba wakati huo timu ikiwa chini ya kocha Abdallah Kibadeni.
Akizungumzia kulikosa taji la Ligi Kuu NBC, Ally alisema msimu huu ubingwa umeamuliwa na dakika 45 za kipindi cha pili cha mechi ya mwisho wakati msimu uliopita timu hiyo ilipigania nafasi ya tatu.
Aliongeza kuwa hata pointi walizofikisha msimu huu (78) hawajawahi kuzifikisha kwa kipindi cha miaka minne iliyopita hivyo walipotoka na walipo ni tofauti na kwamba mwangaza wa mafanikio haupo mbali.
Kuhusu kulikosa taji la ligi kuu kwa misimu minne huku mahasimu wao Yanga wakilibeba mfululizo, Ally alisema wamewahi kukaa miaka mitano bila taji hilo kuanzia 2012 hadi 2017 lakini 2018 walijipanga na kubeba taji hilo miaka minne mfululizo.
Akizungumzia masimango ambayo mashabiki wa Simba wanayapata kwa Yanga baada ya kupoteza mechi hiyo maarufu Dar au Kariakoo Derby mara tano, alisema bado hilo halitoshi kuwafanya wajidharau kwa kuwa hata Real Madrid wamepoteza El Classico nne.
“Hata Real Madrid wamepoteza El Classico nne dhidi ya Barcelona, tena kwa vipigo vikali lakini katu huwezi kuwaona Madrid wakijitukana,” alisema Ally.
Alifafanua kuwa japo si jambo la kujivunia lakini nyakati hizo kwenye mpira hutokea na kuitaja Man United ambayo imelikosa taji la Ligi Kuu England kwa mwaka wa 13 sasa.
“Mifano hii itupe taswira kuwa hatuko peke yetu kwenye mapito ya namna hii na hata hawa wanaotucheka sasa yapo magumu waliyopitia,” alisema Ally.
Aliwataka wana Simba wawape nafasi viongozi wafanye tathmini na baada ya hapo watoe muongozo kuhusu timu hiyo itakavyokwenda mbele katika kuipambania Simba.
Soka Ahmed Ally: Simba hatujafeli
Ahmed Ally: Simba hatujafeli
Read also
