Na mwandishi wetu
Yanga imemchapa hasimu wake Simba au Mnyama mabao 2-0 katika mechi ya mwisho ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa leo Jumatano Juni 25, 2025 na kufanikiwa kubeba moja kwa moja taji la ligi hiyo kwa mara ya nne mfululizo.
Ushindi huo uliopatikana kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam unaifanya Yanga kubeba taji la msimu huu wa 2024-25 ikiwa na pointi 82 na kuiacha Simba nafasi ya pili ikiwa na pointi 78.
Alikuwa ni Pacome Zouzoua aliyeanza kuzamisha jahazi la Simba dakika ya 66 kwa bao la mkwaju wa penalti baada ya kuchezewa ndivyo sivyo na kipa wa Simba, Mousa Camara.
Pacome alikuwa wa kwanza kuuchukua mpira huo na kuuweka katika eneo sahihi kabla ya kupiga kiufundi na kumhadaa kipa Camara ambaye alikuwa kama aliyevurugwa na kujikuta akiuangalia mpira ukiingia wavuni kwa upande wake wa kushoto.
Yanga waliandika bao la pili katika dakika ya 86 mfungaji akiwa Clement Mzize, kwa mara nyingine juhudi za Pacome zilionekana kwa namna alivyotoa pasi iliyozaa bao hilo.
Simba ndio walioanza mapema kulisakama lango la Yanga, dakika ya pili baada ya Khalid Aucho kuporwa mpira lakini Steven Mukwala aliyefanya kazi hiyo alishindwa kuutumia mpira huo kuipatia timu yake bao.
Yanga nao wakajibu mapigo dakika mbili baadaye, Shedrack Boka aliambaa na mpira kabla ya kupiga krosi iliyofika eneo la kipa Camara lakini utulivu wa mabeki wa Simba ukasaidia kuepusha madhara kwenye lango la timu hiyo.
Dakika ya 11, Mudathir Yahya alionesha ubora wake baada ya kumzunguka Chamou Karaboue na kupiga pasi iliyomkuta Prince Dube ambaye alimpasia Pacome lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.
Yanga waliendelea na mashambulizi safari hii dakika ya 18, Israel Mwenda alipiga krosi ambayo ilimkuta Boka lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Mashambulizi hayo yaliendelea hadi kipindi cha kwanza kinamaliza na Simba kuanza kipindi cha pili kwa mabadiliko wakimtoa Joshua Mutale na nafasi yake kuingia Kibu Denis na baadaye kumtoa Kagoma na nafasi yake kuingia Abdulrazak Hamza na Mukwala ambaye nafasi yake aliingia Leonel Ateba.
Mabadiliko hayo yaliimarisha Simba ambayo ilianza kufanya mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Yanga mfano dakika ya 60 Elly Mpanzu alifumua shuti ambalo lilitoka sentimita chache nje ya lango la Yanga.
Yanga nayo ilifanya mabadiliko kadhaa ikiwamo kumtoa Mudathir, Pacome, Dube na Duke Abuya na nafasi zao kuchukuliwa na Clatous Chama, Mzize, Salum Aboubakar na Jonathan Ikangalombo.
Ushindi wa Yanga unakuwa umemaliza mijadala na mizozo iliyotawala kwa takriban miezi mitatu sasa tangu kuahirishwa mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa Machi 8 lakini ikaahirishwa hadi Juni 15 kabla ya kuahirishwa tena hadi Juni 25.
Mijadala hiyo miongoni mwa mashabiki ikiwamo kutokuwa na imani na waamuzi wa Tanzania, inaaminika kuwa sababu ya TFF kuchukua uamuzi mgumu wa kuwapa mechi hiyo waamuzi kutoka nchini Misri walioongozwa na Amin Mohammed Omar aliyekuwa mwamuzi wa kati.
Soka Yanga yaua Mnyama, yabeba taji ligi kuu
Yanga yaua Mnyama, yabeba taji ligi kuu
Read also
