Charlotte, Marekani
Benfica ya Ureno imewaduwaza vinara wa Bundesliga, Bayern Munich kwa kuwachapa bao 1-0 katika mechi ya michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu inayoendelea Marekani.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano hii, bao hilo pekee la Benfica lilipatikana dakika ya 13 mfungaji akiwa Andreas Schjelderup akiitumia krosi ya beki Fredrik Aursnes.
Bayern ambao tayari wamefuzu hatua ya pili ya michuano hiyo, hawakupanga kikosi chao bora na hivyo haikushangaza timu hiyo kuonekana dhaifu na kushindwa kufanya shambulizi la maana hasa kipindi cha kwanza.
Kocha wa Bayern, Vincent Kompany hata hivyo hakuzungumzia udhaifu wa kikosi chake kuwa sababu ya kushindwa badala yake alilaumu hali ya hewa ya joto na aina ya uwanja.
“Nilijua kikosi changu kitapata tabu, nafikiri kipindi cha kwanza hatukuwa bora kabisa, kutokana na hali ya joto na aina ya uwanja, nilihofu kwamba jambo hilo lingeathiri kasi yetu uwanjani,” alisema Kompany.
Baada ya matokeo hayo, timu hizo zitajiandaa kwa hatua ya 16 bora mechi zitakazochezwa siku tano zijazo kwa Bayern kuikabili Flamengo ya Brazil na Benfica kuumana na Chelsea.
Katika mechi nyingine, Chelsea ilitoka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya ES Tunis ya Tunisia.
Ushindi huo umekuwa neema kwa nyota mpya wa Chelsea, Liam Delap ambaye alifunga bao lake la kwanza na timu yake hiyo mpya.
Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Tosin Adarabioyo na hiyo mpya kabla ya kuongeza la pili wakati bao jingine lilifungwa na Tyrique George.
