Na mwandishi wetu
Vinara wa Ligi Kuu NBC, Yanga wameendelea kutoa dozi ya mabao matano baada ya leo Jumapili Juni 22, 2025 kutoka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Hii inakuwa mara ya pili mfululizo kwa Yanga kupata ushindi kama huo katika mechi ya ligi hiyo baada ya Jumatano iliyopita kuilaza Prisons mabao kama hayo.
Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 79 na imebakiwa na mchezo mmoja ambao utapigwa Jumatano ijayo dhidi ya mahasimu wao Simba na wakishinda au kutoka sare watatawazwa mabingwa wa ligi hiyo msimu huu wa 2024-25.
Yanga ilianza kuandika bao la kwanza kupitia kwa Clatous Chama kwa pasi ya Clement Mzize, bao ambao lilidumu kwa dakika 45 za mwanzo na hivyo kutoonesha dalili zozote za timu hiyo kupata ushindi mkubwa.
Mambo yalianza kuwaendea kombo Dom Jiji kipindi cha pili baada ya Yanga kuandika bao la pili lililofungwa na Duke Abuya kwa pasi ya Chama, bao lililofungwa dakika tano baada ya mapumziko.
Kasi ya Yanga iliendelea na kufanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Ibrahim Bacca akiutumia vizuri mpira uliopigwa na Maxi Nzengeli.
Dom Jiji walijikuta wakifungwa mabao mawili katika dakika za lala salama, moja beki wao Joash Onyango alijifunga wakati akiokoa mpira uliopigwa na Farid Musa wakati bao la tano lilifungwa na Nzengeli akimalizia pasi ya Jonathan Ikangalombo.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Simba nayo ilitoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar huku bao hilo pekee likifungwa na Steven Mukwala.
Kwa ushindi huo Simba wamefikisha pointi 78 wakiwa wamebakiwa na mchezo mmoja wao dhidi ya Yanga ambao umebeba hatma ya nani atakuwa kinara wa ligi hiyo msimu huu.
Matokeo ya mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa leo ni kama ifuatavyo…
Namungo 5-0 Ken Gold
Coastal Union 1-1 Tabora United
Fountain Gate 2-3 Azam FC
Pamba FC 1-1 KMC
Singida BS 3-3 Prisons
Mashujaa 0-0 JKT Tanzania
Soka Yanga yaendeleza dozi za 5-0
Yanga yaendeleza dozi za 5-0
Read also
