Miami, Marekani
Kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso ametaka kuwapo uvumilivu baada ya timu yake kutoka sare ya bao 1-1 na Al Hilal katika mechi ya kwanza ya michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu.
Alonso ambaye ndio kwanza amejiunga na timu hiyo akitokea Bayer Leverkusen ya Ujerumani amesema itachukua muda kufanyia kazi mabadiliko anayoyataka katika timu hiyo.
Real Madrid ilikuwa na wakati mgumu mapema katika nusu ya kwanza ya mechi hiyo kabla ya mshambuliaji wao mpya, Gonzalo Garcia kuipatia timu hiyo bao la kuongoza dakika ya 34.
Ruben Neves aliisawazishia Al Hilal kwa mkwaju wa penalti na Real Madrid nayo ilipata fursa kama hiyo ya kuongeza bao la pili ilipopata penalti lakini mkwaju uliopigwa na Federico Valverde uliokolewa na kipa Yassine Bouno.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Alonso alisema kipindi cha pili timu yake ilikuwa bora lakini kipindi cha kwanza walikosa mambo mengi ikiwamo uwiano na tayari wamelizungumza jambo hilo.
“Nilipenda jinsi wachezaji walivyobadilika, tulikuwa na uwezo wa kubadili kasi yetu na kuutawala zaidi mchezo huku tukicheza kwenye eneo lao zaidi, hii ni hatua ni lazima tuichukue vizuri na kuendelea kutafuta ubora,” alisema Alonso.
Alonso alifanya mazoezi kwa mara ya kwanza na kikosi cha Real Madrid, Juni 9 kabla ya kuelekea Marekani kwa ajili ya michuano ya klabu ya dunia inayoendelea nchini humo.
“Nilijua itachukua muda, kuna mambo ambayo tunahitaji kubadilika, kwa pamoja tunahitaji kubadili mambo na tutaendelea kufanya hivyo, kila kitu kinahitaji muda, tuna siku tisa na baadhi ya wachezaji wamefanya mazoezi mara tatu, tuko katika mashindano lakini pia tunataka kujifunza na tunachotaka kukifanya kitachukua muda,” alisema Alonso.
Kipa wa timu hiyo, Thibaut Courtois alisema awali walikuwa na kocha Carlo Ancelotti kwa miaka minne na walimzoea na sasa wanalazimika kubadilika na kufuata anachotaka kocha mpya na hilo halikamilishwi kwa siku nne.
Katika mechi hiyo, Real Madrid ilimkosa mshambuiaji wao nyota, Kylian Mbappe ambaye anasumbuliwa na homa, Mbappe msimu uliopita wa 2024-25 aliifungia timu hiyo mabao 43 katika mashindano yote.
