Philadelphia, Marekani
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amemteua Bernardo Silva (pichani) kuwa nahodha mpya wa timu hiyo licha ya mchezaji huyo kuwahi kusema kwamba huu utakuwa msimu wake wa mwisho na timu hiyo.
Katika kuteua nahodha wa timu, Pep ana kawaida ya kuwahusisha wachezaji na maofisa wa timu kupiga kura na nani wa kumpa wadhifa huo lakini safari hii ameamua kumteua Silva ambaye wasaidizi wake watakuwa Rodri na Erling Haaland.
Silva ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Ureno aliwahi kusema kwamba hana mpango wa kuongeza mkataba Man City wakati mkataba wake wa sasa unafikia mwisho mwakani.
Katika siku za karibuni, Silva ambaye alijiunga na Man City mwaka 2017 akitokea Monaco, amekuwa akihusishwa na mipango ya kurejea katika timu yake ya utotoni ya Benfica ya nchini Ureno.
Akizungumzia uteuzi huo, Silva mwenyewe alisema anajua atakachofanya lakini huu si wakati wa kulizungumzia jambo hilo badala yake mkazo ameuweka katika msimu wake nia ikiwa ni kufanya vizuri kwa ajili ya Man City.
“Wakari ukifika nitalizungumzia hili, nina mwaka mmoja katika mkataba wangu, kwa hiyo ni dhahiri kwamba nitaondoka msimu ujao,” alisema Silva ambaye hucheza nafasi ya kiungo au winga.
Kyle Walker alikabidhiwa majukumu ya unahodha wa timu mwaka mmoja uliopita lakini Pep alisema baada ya kujitokeza mambo asiyoyapenda msimu uliopita ambao ulikuwa wa hovyo hivyo akachukua uamuzi usio wa kawaida ya kuteua nahodha wa timu.
“Mimi ndio kocha na msimu huu kwa mara ya kwanza katika kazi yangu nimeamua nani atakuwa nahodha wangu, sikupenda kilichotokea msimu uliopita, kwa hiyo nimefanya maamuzi msimu huu,” alisema Pep.
Kwa upande wa Walker ametimkia AC Milan wakati Haaland anakuwa nahodha msaidizi kwa mara ya kwanza huku ikikumbukwa kwamba Januari mwaka huu alisaini mkataba wa miaka 10 na Pep anaamini kuna siku Haaland atakuwa nahodha mkuu wa timu hiyo.
“Erling Haaland bado mdogo lakini anatakiwa kuanza kujifunza nini inamaanisha kuwa nahodha kwa sababu matumaini yaliyopo ni kwamba atakuwa hapa kwa miaka mingi, siku zijazo atapewa jukumu la unahodha kwa mara ya kwanza,” alisema Pep.
