Na mwandishi wetu
Kamati ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeitupa rufaa iliyowasilishwa kwao na Guinea dhidi ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’
Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyopatikana leo Jumatatu Juni 16, 2025 ilieleza kuwa Guinea walikata rufaa kupinga uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya CAF kuyatupa malalamiko yao dhidi ya Taifa Stars.
Katika malalamiko yao Guinea waliilalamikia Taifa Stars kwa kumchezesha mchezaji Ibrahim Ame aliyeingia kipindi cha pili katika mechi baina ya timu hizo ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika iliyochezwa Novemba mwaka jana.
Guinea walidai kuwa mchezaji huyo aliingia uwanjani akiwa amevaa jezi yenye namba tofauti na ile iliyoandikwa kwenye orodha rasmi ya wachezaji.
Katika mechi hiyo, Stars walishinda kwa bao 1-0 ambapo Guinea katika hoja zao CAF wamedai kuwa kitendo hicho cha tofauti ya jezi kiliwachanganya kisaikolojia na kuwa sababu ya wao kushindwa mechi hiyo.
Kamati ya Rufaa ya CAF katika maamuzi yake imekubaliana na maamuzi ya Kamati ya Nidhamu kwa madai kwamba hoja za Guinea hazina mashiko kikanuni.
Kimataifa Rufaa ya Guinea dhidi ya Stars yakwama CAF
Rufaa ya Guinea dhidi ya Stars yakwama CAF
Read also