Na mwandishi wetu
Hatimaye Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuusogeza mbele mchezo wa mahasimu wa soka nchini Yanga na Simba ambao sasa utapigwa Juni 25, 2025 badala ya Juni 15 ya awali.
Taarifa hiyo imekuja wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu mechi hiyo ambayo awali ilipangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu kabla ya kuahirishwa hadi Juni 15 lakini sasa imeahirishwa tena hadi Juni 25.
Kama mechi hiyo itachezwa Juni 25 maana yake itakuwa imepita miezi mitatu na siku 16 tangu tarehe ya awali ya mechi hiyo yenye kuvuta hisia za mashabiki wa soka ndani na hata nje ya nchi.
Taarifa hiyo hata hivyo haikuwa na maelezo marefu badala yake ilitaja tarehe ya mechi na kufafanua kuwa itapigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 alasiri na TPLB kuzitakia kila la heri timu hizo katika maandalizi ya mechi hiyo.
Haijaweza kueleweka mara moja timu hizo zitakuja na uamuzi gani baada ya tarehe hiyo mpya kutangazwa hasa kwa Yanga ambao awali walisema hawako tayari kucheza na Simba na kuweka masharti kadhaa kwa TPLB na TFF.
Hatua ya TPLB kuahirisha mechi Machi 8 kwa sababu zilizotajwa kuwa ni za kiusalama baada ya Simba kudaiwa kuzuiwa kufanya mazoezi siku moja kabla ya mechi hiyo ilizua mjadala huku Yanga wakitishia kutocheza mechi hiyo katika tarehe nyingine.
Suala hilo liliingiza bungeni na kusababisha malumbano yasiyo rasmi na yaliyo rasmi miongoni mwa wabunge ambapo baadhi wanaoaminika kuwa ni wa Yanga walisisitiza kutocheza mechi hiyo
Juhudi mbalimbali zilifanyika na kuwahusisha viongozi wakiwamo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na viongozi wa serikali kwa lengo la kutaka mechi hiyo ichezwe lakini Yanga walishikilia msimamo wa kutokuwa tayari kucheza.
Kikao cha mwisho kilifanyika hivi karibuni kati ya viongozi wa TPLB na wale wa Yanga lakini mara tu baada ya kikao hicho, msimamo wa Yanga kutocheza mechi hiyo uliwekwa wazi.
Soka Simba, Yanga sasa ni Juni 25
Simba, Yanga sasa ni Juni 25
Read also