Liverpool, England
Mabingwa wa Ligi Kuu England (EPL) Liverpool, wamekubali kumsajili kiungo mshambuliaji Florian Wirtz (pichani juu) kutoka Bayer Leverkusen ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 100 milioni.
Ada ya mchezaji huyo ambaye ndio kwanza ana miaka 22, imeweka rekodi kwa klabu ya Liverpool wakati kwa England ni CHelsea iliyoweka rekodi ya juu mwaka 2023 ilipomsajili Enzo Fernandez kutoka Benfica kwa ada ya Pauni milioni 107.
Hadi kumpata Wirtz, Liverpool ililazmika kushindana na Chelsea ambao walionesha nia ya kumtaka mchezaji huyo kama ilivyokuwa kwa Bayern Munich ambao nao walitajwa kumtaka.
Wirtz hata hivyo inaaminika aliweka wazi msimamo wake wa kuitaka Liverpool ambao walianza majadiliano na Leverkusen na kufikia muafaka licha ya klabu hiyo kuwasilisha ofa ya awali ya Pauni 126 milioni.
Kabla ya kujiunga na Leverkusen mwaka 2020, Wirtz ambaye pia ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 31 na kuifungia mabao saba, aliwahi kuzichezea timu za SV Grün-Weiß na FC Cologne za Ujerumani.
Akiwa na Leverkusen ameifungia timu hiyo mabao 57 katika mechi 197 na mwaka 2024 alitoa mchango mkubwa kwa timu hyo hadi kubeba taji la Ligi Kuu Ujerumani maarufu Bundesliga.
Kwa sasa Liverpool pia ipo katika mpango wa kumsajili beki wa kushoto wa Bournemouth, Milos Kerkez kwa ada inayotajwa kufikia Pauni milioni 45.
Wakati huo huo, klabu ya Real Madrid ya Hispania nayo inadaiwa kukamilisha usajili wa kinda wa River Plate ya Argentina, Franco Mastantuono (pichani chini) ambaye ni kiungo na mshambuliaji.
Mastantuono, 17, kwa sasa yuko nchini Marekani na klabu yake ya River Plate ambayo ataiwakilisha kwenye michuano ya Fifa ya Klabu ya Dunia itakayoanza kutimua vumbi Jumapili Juni 15, 2025 nchini Marekani.

Real Madrid ilionesha nia ya kumtaka nyota huyo takriban miaka miwili iliyopita kabla ya kuamua kukamilisha mpango huo mwaka huu wakati klabu kadhaa Ulaya ikiwamo PSG nazo zikidaiwa kumtolea macho.
Mastantuono ambaye Agosti 14 mwaka huu atatimiza miaka 18, atajiunga rasmi na timu yake hiyo mpya miezi miwili ijayo tayari kwa ajili ya msimu mpya wa 2025-26.
Mchezaji huyo ambaye ni mzaliwa wa jimbo la Buenos Aires, Juni 5 mwaka huu aliichezea kwa mara ya kwanza timu yake ya taifa ya Argentina katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Chile, mechi ambayo Argentina ilishinda kwa bao 1-0.
