Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola hajampa nafasi kiungo wake wa bei mbaya, Jack Grealish katika wachezaji watakaoshiriki fainali za Kombe la Dunia la Klabu nchini Marekani.
Uamuzi wa Pep kumuweka kando kiungo huyo mshambuliaji aliyemnunua kutoka Aston Villa kwa ada iliyotajwa kufikia Euro milioni 100 umefanyika huku nyota wapya waliosajiliwa na kocha huyo wakipewa nafasi.
Pep katika orodha iliyopatikana jana Jumatano aliwajumuisha nyota hao wapya wakiongozwa na Tijjani Reijnders, Rayan Ait-Nouri na Rayan Cherki.
Grealish, 29, alijiunga na Man City Agosti, 2021 na kusaini mkataba wa miaka sita, anamudu vyema nafasi za kiungo mshambuliaji na winga na zipo taarifa kuwa anawindwa na klabu kadhaa za England na Ulaya.
Klabu mojawapo ambayo imeonesha utayari wa kumtaka nyota huyo wa timu ya taifa ya England ni Everton ambayo itachuana kuiwania saini yake na klabu nyingine barani Ulaya.
Pep aliwahi kusema kwamba Grealish yuko huru kuihama timu hiyo kwa lengo la kusaka nafasi ya uhakika katika kikosi cha kwanza kwenye timu nyingine.
Man City imepangwa kuumana na Wydad AC ya Morocco katika mechi yao ya kwanza ya Kombe la Dunia la Klabu itakayopigwa Juni 18 mjini Philadelphia.
Wachezaji wengine ambao Pep amewaacha katika orodha yake ni Kyle Walker ambaye alikuwa AC Milan kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu na James McAtee ambaye anaiwakilisha timu ya vijana chini ya miaka 21 ya England.
Orodha kamili ya wachezaji wa Man City watakaokwenda Marekani ni pamoja na Stefan Ortega, Marcus Bettinelli na Éderson ambao ni makipa.
Mabeki ni Manuel Akanji, Abdukodir Khusanov, Rico Lewis, Vitor Reis, Josko Gvardiol, Rúben Dias, John Stones, Nathan Aké na Rayan Ait-Nouri,
Viungo: Nico Gonzalez, Rodri, Tijjani Reijnders, Matheus Nunes, Ilkay Gündogan, Rayan Cherki, Bernardo Silva, Claudio Echeverri, Phil Foden, Oscar Bobb na Nico O’Reilly na washambuliaji ni Erling Haaland, Savinho, Omar Marmoush na Jeremy Doku.
Kimataifa Pep amuweka kando Grealish
Pep amuweka kando Grealish
Related posts
Read also
