Munich, Ujerumani
Hatimaye klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) kwa mara ya kwanza imebeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiweka rekodi ya kipekee kwa kuibugiza Inter Milan mabao 5-0.
Ushindi huo uliopatikana Jumamosi hii Mei 31, 2025 kwenye dimba la Allianz Arena mjini Munich utabaki katika kumbukumbu ya kuwa ushindi mkubwa kupatikana katika mechi ya fainali ya michuano hiyo tangu mwaka 1956.
PSG, timu iliyopiganiwa kwa jeuri ya fedha kwa kusajili wachezaji wa bei mbaya kwa lengo la kusaka mafanikio hatimaye imeyapata mafanikio hayo ikimaliza msimu huu na mataji matatu yaani treble, mataji mengine ni lile la Ligi 1 na Coupe de France.
Alianza Achraf Hakimi kwa kufungua ukurasa wa mabao dakika ya 12 dhidi ya timu yake ya zamani na kufuatiwa na mabao mengine mawili kutoka kwa Desire Doue, mshambuliaji kinda mwenye umri wa miaka 19.
Mabao mengine mawili katika ushindi huo wa kihistoria yalifungwa na Khvicha Kvaratskhelia na Senny Mayulu aliyeingia akitokea benchi.
Ushindi wa PSG umekuja baada ya miaka takriban 10 baada ya bilionea wa Qatari kuinunua timu hiyo na kuanza kufanya usajili wa fujo kwa kuwabeba mastaa kibao kwa bei mbaya.
Katika orodha ya mastaa hao walikuwamo kina Neymar, Lionel Messi, Zlatan Ibrahimovic, Kylian Mbappe na wengineo lakini hawakuweza kuipa timu hiyo taji la hadhi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Miaka miwili iliyopita, PSG iliachana na utaratibu wa kusajili mastaa hao badala yake ikawekeza kwa wachezaji wa umri mdogo ambao hatimaye wamewapa taji ambalo wamekuwa wakilisaka kwa muda mrefu.
Kwa ushindi huo PSG inakuwa timu ya pili ya Ufaransa kubeba taji hilo lenye hadhi ya juu na utajiri kati ya mashindano ya klabu Ulaya na duniani, timu nyingine ni Marseille ambayo ilifanya hivyo mwaka 1993.
Kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Luis Enrique hii inakuwa mara yake ya pili kubeba taji hilo baada ya kufanya hivyo akiwa na Barcelona mwaka 2015.
“Tumeweka historia, tumeandika majina yetu katika historia ya hii klabu, kwa muda mrefu hiki ndicho kitu ambacho klabu hii ilipaswa kukipata, tuna furaha, tumetengeneza familia kubwa,” alisema Hakimi.
Kimataifa PSG yabeba taji la kwanza ligi ya mabingwa
PSG yabeba taji la kwanza ligi ya mabingwa
Read also
