Fenerbahce, Uturuki
Kocha wa zamani wa Man United, Jose Mourinho amesema timu hiyo imefanya jambo sahihi kuamua kuendelea na kocha wao Ruben Amorim licha ya kutopata mafanikio msimu huu.
Man United chini ya Amorim msimu huu wa 2024-25 imemaliza Ligi Kuu England (EPL) ikiwa nafasi ya 15, rekodi ambayo ni mbaya na imewanyima nafasi kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Timu hiyo pia imekosa nafasi hiyo baada ya kushindwa kutamba mbele ya Tottenham katika fainali ya Europa Ligi baada ya kulala kwa bao 1-0 kwenye mechi ya fainali.
Akizungumzia mazingira hayo, Mourinho alisema anajua kitendo cha kukosa taji la Europa ni pigo kubwa kwa timu hiyo hasa kwa kuwa imepitia kipindi kirefu bila ya kubeba taji la Ulaya.
Mourinho ambaye mwaka 2017 aliiwezesha Man United kubeba taji la mwisho Ulaya hata hivyo alisema kwamba inaonekana Amorim anaungwa mkono na wanampa muda na mazingira ya kusonga mbele.
Amorim ambaye aliachana na Sporting CP ya Ureno, Novemba mwaka jana na kuanza kibarua cha kuinoa Man United, aliomba radhi kwa mashabiki wa timu hiyo baada ya kumaliza EPL wakiwa nafasi ya chini.
Kocha huyo hata hivyo baada ya kupoteza taji la Europa alisema jambo hilo litakuwa sababu ya kuisaidia timu hiyo iwe bora msimu ujao.
“Nimesoma baadhi ya kauli zake (Amorim) akisema kwamba ana furaha kujiunga na timu hiyo na tayari amepitia katika miezi sita jambo ambalo naweza kulifananisha na kile nilichowahi kupitia,” alisema Mourinho.
Mourinho alisema alipojiunga na FC Porto alikutana na hali kama hiyo, “Nilikwenda Januari 2002 nilikuwa na miezi sita migumu, tulikuwa tunapambana japo tufuzu Kombe la Uefa na tukafanikiwa na baada ya hapo nini kilitokea?” Alisema Mourinho na kuhoji.
Mourinho baadaye aliiwezesha Porto kubeba mataji matatu (treble) akianzia taji la Ureno, Kombe la Uefa, baadaye akabeba taji la ligi kuu na kulitetea kabla ya kuongeza na taji la Ligi ya Mabingwa ulaya katika msimu wake wa kwanza wa 2003-04.
Mourinho ambaye kwa sasa ni kocha wa Fenerbahce pia amewahi kuzinoa timu za Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Tottenham na AS Roma.
