Na mwandishi wetu
Bao pekee la Steven Mukwala limeiwezesha Simba kutoka na pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu NBC dhidi ya Singida BS iliyopigwa leo Jumatano, Mei 28, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Mukwala alifunga bao hilo dakika ya 42 akiitumia pasi ya Jean Ahoua kabla ya kufumua shuti kali baada ya kuwapangua mabeki wa Singida na kipa Amos Obasogi ambaye alitoka golini.
Simba walianza kulisakama lango la Singida mapema dakika ya 24 lakini Joshua Mutale alishindwa kuitumia vizuri krosi ya Shomari Kapombe kuipa Simba bao la kuongoza.
Singida walijibu mapigo dakika 10 baadaye kwa Vicoria Adebayor aliyeufumania mpira akiwa nje kidogo ya eneo la penalti lakini shuti alilopiga lilitoka nje.
Dakika ya 59, Singida walifanya shambulizi jingine baada ya Jonathan Sowah kuyatumia makosa ya Joshua Mutale aliyepoteza pasi ya Ahoua.
Sowah baada ya kuinasa pasi hiyo aliukokota mpira na kufumua shuti ambalo hata hivyo kipa wa Simba, Musa Camara alilidaka.
Simba nao walifanya shambulizi kali dakika ya 65 baada ya Mutale na Mukwala kugongeana wakiwa eneo la Singida na Mutale kufumua shuti ambalo kipa Obasogi aliokoa na mpira kumkuta Shomari Kapombe ambaye alifumua shuti kali lililopaa.
Timu zote zilifanya mabadiliko kadhaa ambayo hata hivyo hayakuweza kubadili matokeo ya mechi hiyo iliyokuwa na rabsha za hapa na pale zilizomlazimu mwamuzi kutoa kadi za njano.
Camara alipewa kadi ya njano kwa kile kilichoonekana kuwa ni kuchelewesha muda baada ya kuanguka chini na kutibiwa kwa muda mrefu wakati Sowah wa Singida alipewa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Camara.
Kwa ushindi huo Simba sasa inakuwa imefikisha pointi 72 katika mechi 27 ikiwa imezidiwa na vinara wa ligi hiyo ambao pia ni mahasimu wao Yanga, kwa tofauti ya pointi moja.
Kwa msimamo ulivyo mechi ya Simba na Yanga iliyopangwa kupigwa Juni 15 ndiyo iliyobeba hatma ya ubingwa wa ligi hiyo msimu huu wa 2024-25.
Kimataifa Mukwala aitungua Singida BS
Mukwala aitungua Singida BS
Read also
