Na mwandishi wetu, Zanzibar
Simba yakwama, ndicho kilichotokea leo Jumapili Mei 25, 2025 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya kushindwa kubeba taji la Shirikisho Afrika mbele ya RS Berkane ya Morocco ambao wamelibeba rasmi taji hilo.
Hadi dakika 90 za mchezo huo wa pili wa fainali zinakamilika Simba na Berkane walitoka uwanjani wakiwa sare ya bao 1-1, matokeo yaliyotosha kuipa Berkane ushindi wa jumla wa mabao 3-1.
Hiyo ni baada ya timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-0 Jumamosi iliyopita wakiwa nyumbani Morocco katika mechi ya kwanza ya fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.
Katika mechi ya leo Simba ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Joshua Mutale akiitumia vizuri krosi ya chini chini ya Elly Mpanzu.
Mpanzu akiwa katika eneo la Berkane aliambaa na mpira ambao ilitarajiwa angefumua shuti badala yake akapiga krosi iliyowapita wachezaji kadhaa wa Berkane na kumkuta Mutale aliyeujaza wavuni.
Simba iliweza kulilinda bao hilo lakini pia timu hiyo ilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga mojawapo ni pale Shomari Kapombe alipokosa bao akiwa karibu na kipa wa Berkane.
Kapombe aliunganisha kwa kichwa krosi ya Mutale lakini mpira alioupiga ulidunda chini na kupaa juu ya lango ukiwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi wasiamini kama wamepoteza nafasi hiyo.
Matumaini ya Simba yakiwa juu baada ya kupata bao na kulilinda kwa kipindi chote cha kwanza, timu hiyo ilipata pigo dakika ya 50 baada ya Yusuf Kagoma kupewa kadi ya pili ya njano (nyekundu) kwa kucheza rafu na hivyo kutolewa nje.
Wakiwa pungufu uwanjani, Simba waliendelea kuwaweka pagumu Berkane wakitengeneza mashambulizi hadi kupata bao dakika ya 73 lililofungwa kwa kichwa na Steven Mukwala aliyeunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Jean Ahoua.
Baada ya mabishano ya dakika kadhaa, bao hilo lilikataliwa na mwamuzi ambaye aliamua kujiridhisha kwa kutumia VAR na kubaini kuwa kuna mchezaji wa Simba aliyeotea kabla ya kufungwa kwa bao hilo.
Pigo la bao kukataliwa lilionekana kuanza kuwauma Simba na kuanza kuruhusu mashambulizi langoni mwao huku Berkane wakitumia wingi wao uwanjani na hatimaye kupata bao dakika ya 90 lililofungwa na Soumaila Sidibe.
Hii ni mara ya tatu kwa Berkane kubeba taji hilo wakati Simba wamekwama kuweka rekodi ya kihistoria ya kulibeba taji hilo kwa mara ya kwanza,
Simba kama wangefanikiwa ingekuwa timu ya kwanza ya Tanzania kubeba taji la michuano ya soka ya klabu Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Baada ya mwaka 1993, hii inakuwa mara ya pili kwa Simba kufikia hatua ya fainali ya michuano ya klabu barani Afrika na kushindwa kubeba taji licha ya kuwa mwenyeji katika mechi ya pili inayotoa bingwa.
Mwaka 1993, Simba ikiwa Uwanja wa Uhuru (Taifa) Dar es Salaam ilishindwa kutamba mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Tukio la mwaka 1993 liliacha huzuni kwa maelfu ya mashabiki wa timu hiyo walishuhudia kombe likienda Ivory Coast kama ilivyokuwa hii leo kwenye Uwanja wa Amaan kwa mashabiki kushuhudia kombe likielekea Morocco.
Kimataifa Simba yakwama, Berkane yabeba taji Shirikisho Afrika
Simba yakwama, Berkane yabeba taji Shirikisho Afrika
Read also