Na mwandishi wetu
Simba imeanza vibaya mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kulala kwa mabao 2-0 mbele ya RS Berkane ya Morocco.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi hii Mei 17, 2025 mjini Berkane kwenye Uwanja wa Manispaa, Simba ilishtushwa kwa bao la dakika ya 8 lililofungwa na Mamadou Camara aliyeuwahi mpira wa kona na kuujaza wavuni kwa kichwa akiwaacha wachezaji wa Simba wakiwa wameduwaa.
Dakika saba baadaye, Simba walifungwa bao la pili mfungaji akiwa Ousamah Lamlawi ambaye aliutumia mpira uliopotea miguuni mwa Yusuf Kagoma na kurudishwa kwenye lango la Simba.
Mpira huo ulianzia kwa kipa Musa Camara aliyeupiga kwa Kagoma lakini Kagoma baada ya kuutuliza ukawahiwa na mchezaji wa Berkane aliyekuwa karibu na kumpasia mfungaji ambaye aliwadaa mabeki wa Simba kabla ya kuujaza wavuni akiwa karibu kabisa na Camara.
Berkane waliendelea kulisakama lango la Simba na dakika ya 61 walipata bao lililofungwa na Yousef Mehr kwa pasi ya Mamadou Camara lakini baada ya kutumia VAR mwamuzi alikataa bao hilo kwa madai kuwa kuna mchezaji wa Berkane aliotea.
Wenyeji Berkane ndio waliouanza mchezo kwa kulisakama lango la Simba ambao wakiwa nyuma kwa mabao mawili walianza kujibu mapigo dakika ya 29 baada ya Shomari Kapombe kupiga krosi ya chinichini lakini mpira huo ulikuwa mwingi hadi kutoka nje baada ya kumshinda Kibu Denis aliyejitahidi kuurudisha uwanjani bila mafanikio.
Dakika ya 42, Simba walipata kona yao ya kwanza baada ya Elly Mpanzu kuwatoka wachezaji wa Berrkane na kufumua shuti lililookelewa lakini kona iliyochongwa na Jean Ahoua haikuwa na madhara.
Dakika ya 23 kocha wa Simba, Fadlu Davids alijikuta akipewa kadi ya njano baada ya kumlalamikia mshika kibendera aliyekuwa karibu na eneo ambalo Ahoua alichezewa ndivyo sivyo lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
Kasi ya Berkane ilionekana kuwa ngumu kwa beki Abdulrazack Hamza wa Simba ambaye aliumia dakika ya 23 na kuomba kutolewa nje na nafasi yake ikachukuliwa na Chemalone Fondoh.
Simba ilikianza kipindi cha pili kwa kumtoa Kibu ambaye nafasi yake aliingia Valentino Nouma na baadaye akatoka Mpanzu na nafasi yake kuingia Joshua Mutale zikiwa zimebaki dakika 10 mpira kumalizika.
Dakika moja baada ya kuingia Mutale aligongeana pasi na Ahoua lakini shuti la Ahoua likapaa juu ya lango na kumuacha kipa wa Berkane, Munir Mohamed akiishia kuuangalia mpira huo kwa tahadhari.
Ahoua naye alitolewa katika dakika nane za nyongeza na nafasi yake kuingia Deborah Fernandes.
Kipigo cha leo kinawakumbusha mashabiki wa Simba mechi yao ya robo fainali ya michuano hiyo dhidi ya Almasry ya Misri ambapo timu yao ikiwa ugenini ililala kwa mabao 2-0.
Baadaye katika mechi ya marudiano kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba ikapata ushindi kama huo kabla ya kusonga mbele hadi nusu fainali kwa ushindi wa penalti 4-1.
Katika hatua ya nusu fainali Simba ilifanikiwa kuitoa Stellenbosch ya Afrika Kusini na ndipo ilipokata tiketi ya kucheza hatua ya fainali dhidi ya Berkane.
Simba itacheza tena na Berkane Mei 25 katika mechi ya pili ya fainali hiyo, mechi ambayo inatarajia kupigwa kwenye Uwanja wa Mkapa au New Amaan Zanzibar.
Mara ya mwisho Simba kufikia hatua ya fainali ya michuano ya klabu Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ilikuwa mwaka 1993 ambapo ilishindwa kutamba mbele ya Stellah Abidjan ya Ivory Coast.
Kimataifa Berkane moto, Simba yalala 2-0
Berkane moto, Simba yalala 2-0
Read also