Liverpool, England
Mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah amesema beki wa timu hiyo Trent Alexander-Arnold (pichani) hakustahili kuzomewa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo.
Beki huyo wa kulia alizomewa Jumapili iliyopita na mashabiki wa timu hiyo iliyobeba taji la Ligi Kuu England (EPL) msimu huu ambao inaaminika hawakufurahishwa na uamuzi wake wa kutangaza kuhamia Real Madrid.
Tukio la kuzomewa kwa beki huyo lilitokea katika mechi dhidi ya Arsenal iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2 ambapo mchezaji huyo aliingia akitokea benchi na ndipo alipokutana na zomeazomea hiyo.
Alexander-Arnold, 26, ni mzaliwa wa Liverpool na klabu hiyo ndiyo iliyomkuza na kwa maera ta kwanza alianza kucheza timu kubwa mwaka 2016 lakini msimu ujao anatarajia kuwa mchezaji mpya wa Real Madrid.
“Nafikiri kwa kiasi fulani mashabiki wamekuwa katili kwake, nafikiri hakustahili kwa wakati ule, alistahili kupewa heshima na mashabiki katika namna bora iwezekanavyo kwa sababu alikuwa akijitoa kwa ajili ya mashabiki,” alisema Salah.
Salah pia alisema kwamba haitakiwi kufanywa hivyo kwa mtu yeyote badala yake inatakiwa kuwe na tabia ya kuwashukuru watu wanaopita katika klabu hiyo hata kwa miezi sita.
Alexander-Arnold ameichezea Liverpool mechi 353 katika mashindano yote na kuifungia mabao 23, ameiwezesha kubeba mataji mawili ya EPL, Ligi ya Mabingwa Ulaya mara moja, FA na Kombe la Ligi mara moja moja.
Salah ambaye pia alisema anampenda beki huyo alisisitiza kwamba mchezaji huyo alitakiwa kuagwa katika namna iliyo bora kwa kuzingatia mambo aliyosaidia kuyafanikisha katika klabu.