Manchester, England
Kiungo wa Man United, Casemiro amepongeza uamuzi wa kumpa kocha Carlo Ancelotti jukumu la kuinoa timu ya taifa ya Brazil akidai kwamba timu hiyo inahitaji kocha mwenye hadhi.
Casemiro anamjua fika Ancelotti, ni kocha ambaye wamekuwa pamoja kwa misimu mitatu katika kikosi cha Real Madrid na walibeba mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na moja la La Liga.
Jumatatu iliyopita Shirikisho la Soka Brazil (CBF) lilitangaza Ancelotti kuanza kibarua cha kuinoa timu hiyo baada ya kuumaliza msimu huu na klabu ya Real Madrid na hivyo kumfanya awe kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu ya Brazil.
Mara baada ya kuanza kibarua hicho kipya, mtihani wa kwanza kwa Ancelotti utakuwa Juni 5 kwa mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ecuador na kufuatiwa na mechi dhidi ya Paraguay siku tano baadaye.
Casemiro, 33, alimsifu Ancelotti akisema ni mtu wa kipekee mwenye hadhi, jina kubwa na mwenye sifa hasa kwa namna ambavyo analizungumzia soka na namna anavyolifahamu soka.
“Baada ya kuondoka kwa Tite nafikiri alitakiwa kuwa yeye (Ancelotti) Brazil inahitaji mtu profesheno kama Ancelotti, Brazil inahitaji jina kubwa kama yeye, inahitaji mtu ambaye atasimamia nidhamu,” alisema Casemiro.
“Nina furaha kocha mwenye hadhi anaifundisha timu ya taifa ya Brazil ila kidogo nasikitika kwa sababu itakuwa ni kwa muda mfupi, nasema hivyo kwa sababu mimi namjua jamaa, tena namjua vizuri,” alisema Ancelotti.
Habari za ndani zinadai kwamba Ancelotti atapewa mkataba utakaofikia ukomo mara baada ya fainali za Kombe la Dunia 2026 ingawa atakuwa na fursa ya kuongeza zaidi ya muda huo.
