Na mwandishi wetu
Simba imeendelea kutembeza vipigo katika Ligi Kuu NBC baada ya leo Jumapili, Mei 11, 2025 kuichapa KMC mabao 2-1 mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Kinondoni, Dar es Salaam.
Kabla ya leo, Simba katika mechi tatu zilizopita za ligi hiyo ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa, bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na 5-1 dhidi ya Pamba Jiji.
Kwa ushindi wa leo timu hiyo inakuwa imefikisha pointi 69 na kuendelea katika nafasi yake ya pili ikiwa imezidiwa na vinara wa ligi hiyo Yanga yenye pointi 70 huku zote zikiwa zimecheza mechi 26.
Wenyeji KMc wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Simba katika dakika ya 10 kwa bao lililofungwa na Rashid Chambo.
Chambo alifunga bao hilo kwa juhudi binafsi baada ya kuinasa pasi akitumia guu lake la kushoto aliukokota mpira na kuuweka sawa kabla ya kufumua shuti la nje ya 18 ambalo lilimshinda kipa Musa Camara.
Simba baada ya kupambana walisawazisha bao hilo dakika ya 20 mfungaji akiwa ni Steven Mukwala ambaye aliitumia pasi ya Joshua Mutale.
Mukwala alipata nafasi mbili za kuifungia Simba, kwanza dakika ya 44 alipigiwa pasi ya juu na Kibu Dennis lakini mpira wa kichwa aliopiga akiwa karibu na lango la KMC ulitoka nje.
Mukwala kwa mara nyingine alikosa bao dakika za nyongeza kabla ya mapumziko, safari hii akiunganishiwa pasi na Mutale lakini umahiri wa kipa wa KMC, Ally Ahmada ulikuwa kikwazo kwa mchezaji huyo kufunga bao licha ya kuwa karibu na lango.
Dakika moja kabla ya mapumziko, Chombo kwa mara nyingine aliisumbua safu ya ulinzi ya Simba kwa kuwazidi ujanja mabeki lakini wakati akielekea kuonana na kipa Camara, Abdulrazack Hamza alimchezea rafu na hapo hapo mwamuzi akampa kadi ya njano.
Mukwala alirekebisha makosa yake dakika ya 46 kwa kuipatia Simba bao la pili na la ushindi kwa mara nyingine akiitumia pasi ya Mutale.
Baada ya mechi ya leo Simba, itasimama katika mechi za ligi kuu ikijiandaa kuivaa RS Berkane ya Morocco katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Jumamosi ijayo ambapo wawakilishi hao wa Tanzania watakuwa ugenini.
Kimataifa Simba yaitandika KMC 2-1
Simba yaitandika KMC 2-1
Read also