Na mwandishi wetu
Mtangazaji wa zamani aliyejipatia umaarufu kwa kutangaza kwa ubora mechi za soka nchini Tanzania, Charles Hllary (pichani) amefariki dunia alfajiri ya leo, Mei 11, 2025.
Charles ambaye hadi umauti unamkuta alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Zanzibar, taarifa za kifo chake zimetolewa katika vyanzo mbalimbali vikiwamo vile vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Taarifa hizo hata hivyo hazikuweka wazi sababu ya kifo cha nguli huyo wa utangazaji ambaye pia alisifika kwa kutamka maneno ya Kiswahili kwa ufasaha na umaridadi.
Wakati wa uhai wake, Charles Hillary alijipatia umaarufu kwa kutangaza vipindi vya michezo enzi hizo zkiwa Radio Tanzania hasa mechi za soka za ligi za ndani na zile za kimataifa.
Katika hilo, Charles alisifiwa kwa namna ambavyo utangazaji wake kwenye redio ulitosha kumfany shabiki ajione kama yuko uwanjani anaangalia mechi moja kwa moja.
Mashabiki wengi wa mpira hasa miaka ya 1980 na 1990 mwanzoni ilikuwa burudani kwao kumsikia Charles akitangaza mechi za Simba na Yanga na nyingine zilizokuwa na ushindani.
Sambamba na vipindi vya michezo, Charles pia alikuwa mahiri kwa usomaji wa taarifa ya habari pamoja na vipindi vya burudani jambo ambalo lilijidhihirisha zaidi alipohamia Radio One.
Enzi hizo akiwa Radio One umahiri wake katika vipindi vya burudani ya muziki ulimfanya abatizwe jina la Mzee wa Macharanga, jina ambalo alidumu nalo kabla ya kuhamia DW na baadaye BBC akifanyia kazi nchini Uingereza.
Alikaa Uingereza kwa kipindi kirefu akiwa na BBC kabla ya kurudi Tanzania na kujiunga na Azam TV ambapo pia alifanya kazi kwa miaka kadhaa na baadaye akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu ya Zanzibar.
Kimataifa Mtangazaji maarufu Charles Hillary afariki dunia
Mtangazaji maarufu Charles Hillary afariki dunia
Related posts
Read also