Paris, Ufaransa
Baada ya Arsenal kutolewa kwenye nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya, kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta amesema timu yake ndiyo iliyokuwa bora kwa asilimia 100 katika michuano hiyo msimu huu.
Arsenal juzi Jumatano katika mechi ya pili ya nusu fainali ya ligi hiyo ilishindwa kutamba ugenini jijini Paris baada ya kuchapwa mabao 2-1 na PSG.
Kwa kipigo hicho Arsenal imeziaga fainali za michuano hiyo ya klabu mikubwa na yenye hadhi Ulaya na duniani kwa kufungwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kulala kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza.
Ikiwa jijini Paris, Arsenal ilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga lakini ilikwama mbele ya kipa Gianluigi Donnarumma kabla ya kupata bao pekee la Bukayo Saka wakati mabao ya PSG yalifungwa na Fabian Ruiz na Achraf Hakimi.
Akizungumzia ubora wa timu yake, Arteta alisema kwamba walikuwa karibu sana kwenye kupata mafanikio katika michuano hiyo kuliko ambavyo matokeo yamekuwa lakini bahati mbaya wametolewa.
“Najivunia wachezaji kwa asilimia 100, sidhani kama kuna timu ambayo imekuwa bora kuzidi hii (Arsenal) katika mashindano haya kwa namna ambavyo nimeona lakini ndio hivyo tuko nje,” alisema Arteta.
Arteta pia alisema baada ya timu yake kushindwa kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo, wachezaji wake wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo walikuwa katika hali ya huzuni na wengine wakitokwa machozi.
Arsenal ambao mara yao ya mwisho kufikia hatua ya fainali za michuano hiyo ilikuwa msimu wa 2005-06, kwa kushindwa kufuzu hatua ya fainali maana yake wanamaliza msimu huu bla taji lolote.
Mara ya mwisho Arsenal kubeba taji ilikuwa mwaka 2020 wakati Arteta alipoiongoza vyema timu hiyo kubeba Kombe la FA.