Milan, Italia
Beki wa Barcelona, Inigo Martínez amekana kumtemea mate beki wa Inter Milan, Francesco Acerbi katika tukio linalodaiwa kutokea baada ya Inter kufunga bao la pili katika mechi baina ya timu hizo jana Jumanne.
Barca na Inter ziliumana katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo Inter ilitoka na ushindi wa mabao 4-3 na kujikatia tiketi ya kucheza fainali dhidi ya mshindi wa mechi ya leo Jumatano kati ya Arsenal na PSG.
Tukio lenyewe inadaiwa lilitokea baada ya Hakan Çalhanoğlu kufunga bao la penalti na wakati Acerbi akishangilia alionekana kama akisema kwa ukali mbele ya Martinez ambaye picha zilimuonesha akijibu mapigo katika namna ya kuonesha hasira.
“Alifurahia bao kwenye sikio langu, namna nilivyojibu tukio hilo si jambo la muhimu lakini sikuwa mwenye kumlenga yeye, tukio la kutema mate lilikuwa mbali yake, tofauti na hivyo ningetolewa nje, kwa hakika hilo halina ubishi,” alisema Martinez.
Acerbi ambaye alifunga bao la kusawazisha na kuzifanya timu hizo zicheze dakika 30 za nyongeza, muda mfupi baadaye alilalamika kwa mwamuzi akidai Martinez alimtemea kitu.
Mwamuzi hata hivyo hakuonesha kuguswa mno na tukio hilo ikiwamo kutokuwa tayari kutumia VAR ili kujiridhisha.
Mwisho wa yote, Barca walizamishwa na bao la Davide Frattesi lililofanya matokeo kuwa 4-3 na hivyo Inter kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-6 baada ya sare ya mabao 3-3 katika mechi ya kwanza.
