Na mwandishi wetu
Siku moja baada ya Yanga kutangaza kutocheza mechi yao na Simba, ratiba mpya ya Ligi Kuu NBC imetoka ikionesha kuwa timu hizo mahasimu zimepangwa kucheza Juni 15 mwaka huu.
Ratiba hiyo iliyotolewa leo Jumanne Mei, 6, 2025, pia imeonesha kuwa baada ya mechi hiyo timu hizo kila moja itakuwa na mechi mbili za kumalizia msimu huu wa 2024-25.
Simba itacheza na Ken Gold Juni 18 na kufuatiwa na mechi dhidi ya Kagera Sugar ambayo itachezwa Juni 22 wakati Yanga itacheza na Prisons Juni 18 na kufuatiwa na mechi nyingine dhidi ya Dodoma Jiji itakayopigwa Juni 22.
Kutolewa kwa ratiba hiyo mpya kunazidi kuacha maswali kuhusu majaliwa ya mechi ya mahasimu hao hasa baada ya Yanga kushikilia msimamo wa kutocheza kwa kile wanachodai kuwa ni kupinga dhulma.
Uamuzi huo wa Yanga umekuja baada ya kukwama kwa rufaa yao waliyoiwasilisha Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) wakipinga kuahirishwa ghafla kwa mechi yao dhidi ya Simba iliyopangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu.
Mechi hiyo iliahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya Simba waliokuwa timu mgeni kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mkapa siku moja kabla ya mechi hiyo na watu wanaodaiwa kuwa ni wa Yanga.
Baada ya tukio hilo, Simba walitishia kutocheza mechi hiyo lakini baadaye TPLB walitoa taarifa ya kuifuta mechi hiyo saa chache kabla ya muda wa kuchezwa kwa sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni ya kiusalama.
Taarifa ya bodi hiyo ilieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa kwa kuwa baadhi ya hoja zilizowasilishwa kwao hasa kuhusu usalama zilihitaji muda kwa ajili ya kuchunguzwa kabla ya kutoa uamuzi.
Yanga hawakufurahishwa na uamuzi huo na ndipo walipowasilisha suala hilo CAS ambao katika majibu yao waliwataka kulifikisha suala hilo katika mamlaka za ndani za soka.
Uamuzi huo wa CAS haukukubaliwa na Yanga ambao walidai kwamba hawawezi kulipeleka suala hilo kwenye mamlaka hizo kwa madai kwamba hazitendi haki.
Uamuzi wa kususia mechi hiyo uliofikiwa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo chini ya kiongozi wao, Hersi Said lengo lake limetajwa kuwa ni kupinga dhulma zinazofanywa na mamlaka za soka nchini.
Kimataifa Yanga, Simba Juni 15…
Yanga, Simba Juni 15…
Read also