Rio de Janeiro, Brazil
Shrikisho la Soka Brazil (CBF) linatarajia kumtaja kocha mpya wa timu ya taifa ya soka ya wanaume mwishoni mwa wiki ijayo.
Kwa kipindi kirefu sasa CBF wamekuwa wakielezea kusudio lao la kumpata kocha mpya wa timu hiyo tangu kutimuliwa kwa Dorival Junior, Machi 28, mwaka huu.
Akizungumzia mpango wa kumsaka kocha mpya, mkurugenzi wa timu hiyo, Rodrigo Caetano alisema kwamba wanafahamu kuwa kumchagua kocha wa timu ya taifa ya Brazil ni suala lenye umuhimu wake na lenye kubeba dhima kubwa.
Caetano hata hivyo alisema pamoja na mtazamo huo wanatarajia kufikia uamuzi kuhusu nani atakuwa kocha mpya mwishoni mwa wiki ijayo.
Habari za ndani zinadai kwamba suala la kocha Carlo Ancelotti (pichani) limeingia katika sintofahamu kuhusu muda atakaoachana na Real Madrid, taratibu za kuvunja mkataba pamoja na maslahi ya kocha huyo ambaye ana mkataba na timu hiyo ya Hispania hadi mwaka 2026.
CBF hata hivyo inajua fika kwamba muda wa kujua hatma ya kocha huyo unahusisha moja kwa moja mbio za Real Madrid katika kulisaka taji la Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga.
Real Madrid kwa sasa inashika nafasi ya pili katika ligi hiyo ikiwa imeachwa na vinara na mahasimu wao Barcelona kwa tofauti ya pointi nne huku zikiwa zimebakia mechi nne kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.
Dhamira ya CBF ni kuhakikisha wanampata kocha mpya ambaye ataanza kazi Mei 26 siku ambayo kikosi cha timu hiyo kinatarajia kutangazwa kwa ajili ya mechi mbili za kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ecuador na Paraguay ambazo zitachezwa mapema mwezi Juni.
Kimataifa Kocha mpya Brazil kutajwa wiki ijayo
Kocha mpya Brazil kutajwa wiki ijayo
Read also