Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa PSG, Ousmane Dembele yuko fiti kwa ajili ya mechi ya kesho Jumatano Mei 7, 2025 dhidi ya Arsenal baada ya kupona matatizo ya misuli yaliyokuwa yakimkabili.
Awali, Dembele ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Ufaransa alikuwa katika hatihati ya kucheza mechi hiyo ya nusu fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa kumaliza mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Emirates.
Dembele ambaye ndiye aliyefunga bao pekee na la ushindi katika mechi ya kwanza, alikosa mechi ya Ligi 1 ya PSG na Strasbourg wikiendi iliyopita lakini jana Jumatatu alianza mazoezi.
“Amekuwa akifanya mazoezi nasi kwa siku mbili zilizopita, mlimuona Jumanne (leo) ameshiriki ratiba ya kawaida ya mazoezi na atakuwa uwanjani kwa ajili ya mechi ya Jumatano,” alisema kocha wa PSG, Luis Enrique.
Dembele ambaye alijiunga na PSG mwaka 2023 akitokea Barcelona, kwa sasa ndiye mfungaji wa PSG mwenye mabao mengi msimu huu akiwa amefikisha mabao 33.
Arsenal ambao watakuwa ugenini watatakiwa kuhakikisha wanapata ushindi ili kusonga mbele baada ya kupoteza mechi ya kwanza wakiwa nyumbani.
Timu itakayosonga mbele itaumana katika mechi ya fainali na mshindi wa mechi kati ya Inter Milan na Barcelona ambazo zinaumana usiku wa Jumanne hii.
