Liverpool, England
Beki wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold (pichani) amekataa kusaini mkataba mpya na timu hiyo kwa kinachoaminika kuwa anataka kuondoka huku kukiwa na habari kwamba anaelekea Real Madrid.
Habari zaidi zinadai kwamba katika mpango huo huenda Trent akawa beki wa pembeni atakayekuwa akilipwa fedha nyingi zaidi duniani.
Trent ambaye pia ni beki wa timu ya taifa ya England ataondoka Liverpool akiwa mchezaji huru na ingawa hajatangaza wapi anaelekea lakini kupitia mitandao ya kijamii leo Jumatatu, ameweka wazi kwamba anaondoka Liverpool.
Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii beki huyo alisema kwamba uamuzi ambao ameuchukua haukuwa rahisi kwake na umegubikwa na fikra za mitazamo mbalimbali.
“Awali ya yote niseme huu si uamuzi rahisi na kumekwua na fikra za mitazamo mingi, nimekuwa hapa kwa miaka 20, nimeipenda kila dakika moja ya hapa, nimefanikisha ndoto zangu zote, nimefanikisha kila nilichotaka hapa,” alisema Trent.
Alisema kwamba kujitoa nje ndani kwa miaka 20 kumemfanya afike mahali na kujiwa na fikra kwamba anahitaji mabadiliko mapya na changamoto mpya kwake kama mchezaji na binadamu na anadhani huu ni wakati sahihi kufanya hivyo.
Trent, 26, ambaye mkataba wake Liverpool unafikia ukomo mwisho wa msimu huu, alijiunga na timu hiyo akiwa na miaka sita, hadi sasa ameichezea jumla ya mechi 349 na kuanzia Juni 2023 amekuwa akifanywa nahodha msaidizi.
Kama mpango wa kujiunga na Real Madrid utafanikiwa, akiwa timu hiyo atakuwa anaungana na rafiki na mchezaji mwenzake wa timu ya England, Jude Bellingham.
